Haji Manara aomba radhi hadharani kutokana na sakata la Arusha
Msemaji wa Klabu ya Young Africans Haji Manara amemuomba radhi Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ Wallace Karia, kufuatia tukio lililojitokeza wakati wa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Wawili hao walikwaruzana wakiwa Jukwaa Kuu Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, na baadae picha za video za tukio la mzozo wao kusambaa kwenye Mitandao ya Kijamii.
Manara amesema baada ya tukio hilo, alijitafakari na kubaini alikosea, hivyo alimtafuta Rais Karia na kumuomba radhi jana Jumatatu (Julai 04), wakiwa jijini Dar es salaam.
“Nilichukua muda wangu kujitafakari sana, niliona nimekosea, hivyo nilimtaka Hersi twende kwa Rais na bahati nzuri tulimkuta na nilimuomba radhi kwa kile kilichotokea Arusha.”
“Pia niwaombe radhi wadau wote wa Soka nchini Tanzania waliokwazika na tukio lile, hata nyinyi Waandishi wa Habari ninawaomba radhi kwa sababu ninahisi mlikwazika sana.”
“Ninarudia tena, sikumtukana na wala sikufanya lolote ambalo linaashiria matusi, nimeshangazwa kuona kuna mtu mmoja alinipakazia kwa kuandika nimemtukana Rais wa TFF!” amesema Manara
Hata
hivyo tayari Sekretarieti ya TFF imeshamfungulia Mashtaka Haji Manara kwenye
Kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo, na wakati wowote shitaka hilo litaanza kusikilizwa
na kutolewa hukumu.
No comments
Post a Comment