Header Ads

Header ADS

Mkurugenzi Wa Idara Ya Maendeleo Ya Jamii Ashiriki Ujenzi Wa Maabara

  Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amesema kimsingi jukumu la wataalam wa Maendelaeo Nchini sio tu kutoa mikopo kwa vikundi vya uwezeshaji wananchi kiuchumi bali ni kuchechemua ari ya wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali walizonazo.


















Bw. Golwike amesema hayo leo jiji Dodoma katika Kata ya Iyumbu wakati wa zoezi la wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kushiriki ujenzi wa maabara ya Shule ya Sekondari Iyumbu iliyoko nje kidogo ya Jiji la Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa Wiki ya Mkutano Mkuu wa wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii.
   "Kimsingi jukumu la maafisa maendeleo ya Jamii sio kusimamia na kutoa mikopo peke yake hapana bali ni kuhakikisha wanachechemua wananchi katika kushiriki katika kujiletea maendeleo katika maeneo yao na kushiriki katika miradi ya maendeleo" amesema.
   Bw. Golwike amesema  kuwa ushiriki wa zoezi la ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara ya shule hiyo iliyoendeshwa na wataalam wa sekta ya maendeleo ya jamii ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jamii  ya mwaka 1996 kwa vitendo kwani sera hiyo inawataka wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo.
    Kwa upande wake Afisa Tarafa ya Dodoma Bi. Neema Nyalege, wakati alipokuwa akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Bw. Patrobas Katambi amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhamasisha jamii kujiletea maendeleo bado mwamko wa jamii kutumia rasilimali zilizopo kujiletea maendeleo bado huko chini.
   Ameongeza kuwa kwa wataalam hao kutambua mwitikio huo mdogo kwa jamii ndio maana wameamua kushirikiana na wananchi wa kata ya Iyumbu kujenga maabara hiyo ya vyumba vitatu ili kuamsha ari ya wananchi kushiriki kujiletea maendeleo.
  Pia,Ameitaja hatua hiyo kuwa ya kupongezwa kwani imetekeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996 inayohimiza wananchi kujiletea Maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo.
  Aidha Galwike amewataka wanafunzi shuleni hapo kusoma masomo ya Sayansi ndio maana wataalam hawa wako hapa ili kuchangia ujenzi wa maabara yao kwa lengo la kuwapa hamasa wanafunzi shuleni hapo kusoma sayansi kwa vitendo badala ya nadharia ili hapo baadae waweze kulisaidia taifa katika fani ya sayansi na teknolojia.
    Bi. Janeth David Mkazi wa Kata Ya Ijumbu amewashukuru wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwa kuja kuwaunga mkono juhudi zao za kujenga shule na maabara ili kuwakomboa watoto kutembea umbali wa kilometa 24 kufuata huduma ya elimu katika Shule ya Sekondari Kisasa. 
  Hata hivyo,Wataalamu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii wanakutana Jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wao wa mwaka kwa lengo la kukumbushana majukumu yao lakini pia kupata maarifa mapya kutoka mada mbalimbali zitakazotolewa katika mkutano huo wa siku nne unaotarajia kufanyika.

No comments

Powered by Blogger.