Header Ads

Header ADS

Rais Wa Zanzibar afanya uzinduzi wa Vitambulisho vipya vya Mzanzibar(Smart Cards)

   Dk. Ali Mohamed Shein ambae ni RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,amesema matumizi ya Vitambulisho vipya vya Mzanzibari mkaazi (smart card) yataiwezesha serikali kuweka na kuhifadhi kumbukumbu za matukio ya watu wote katika Daftari la Usajili na Utambuzi. Dk. Shein amesema hayo leo katika uzinduzi wa Kadi mpya za Kielektronik ya Mzanzibari mkaazi, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul wakil Kikwajuni mjini Unguza.
     ambapo ameeleza kutokana na vitambulisho hivyo yataisaida Serikali, taasisi na watu binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbali mbali zenye mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.
     Aidha, alisema kuwepo kwa mfumo huo wa matumizi ya vitambulisho vipya kutaisadia serikali katika kuwatambuwa watu wanaostahiki kupata haki za msingi , kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984. “Itawezesha kumtambua mtu anaestahiki kupata haki yake kama vile malipo ya pensheni, haki za matibabu, kujiunga na masomo na nyenginezo”, alisema.












  

      Dk. Shein amesema, kutokana uwepo wa vitambulisho hivyo Serikali itapata urahisi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato hivyo kuimarisha huduma muhimu za kijamii, ikiwemo afya, elimu, barabara pamoja na ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
    Alieleza kuwa vitambulisho hivyo vimetengenezwa kwa teknolojia ambayo sio rahisi kughushiwa, vikiwa na uwezo mkubwa wa kiusalama wa taarifa za mtumiaji, akibainisha kutumika katika nchi kadhaa duniani. Rais Dk. Shein alitowa wito kwa wakaazi wote wa Zanzibar waliofikia umri wa miaka 18 kwenda kujisajili katika ofisi za Wakala wa Usajili wa matukio ya Kijamii zilizopo katika Wilaya zote nchini, sambamba na wale ambao bado hawajajiandikisha kufanya hivyo.
     Lakini pia, amewataka watendaji wanaohusika na utayarishaji wa vitambulisho hivyo, kuwa makini na waangalifu katika utoaji wake. Vile vile aliwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia vizuri taarifa za uhakiki wa watu walioko katika maeneo yao, kuanzia ngazi za shehiya, wadi na Wilaya ili kuhakikisha wanawatambua wananchi wao na taarifa zao zilizo sahihi. “Ni muhimu mlifanyie mapitio daftari la wakaazi katika shehiya, ambalo ndio msingi wa uthibitisho wa kujua taarifa za utambuzi na makazi ya watu waliomo katika maeneo yenu”, alisema.
    Dk. Shein amewataka wananchi kutambua jukumu la kuisadia Ofisi ya Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii katika kutambuwa wakaazi wa maeneo yao badala ya kuiachia jukumu hilo Ofisi hiyo pekee. Aidha, aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kutumia njia za mkato katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, akibainisha hatua hiyo imekuwa chanzo cha kuibuwa rushwa.
“Naendelea kukunasihini watendaji wote wa Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii Zanzibar, mfanye kazi zenu kwa uadilifu, uzalendo na mfungamane na misingi ya haki na sheria pamoja na kufuata taaribu zilizowekwa katika kuendesha Ofisi ”, alisema.
    Imeripotiwa na Mwandishi wetu;Adolf Mwingira

No comments

Powered by Blogger.