Header Ads

Header ADS

RC Mtaka Awataka TRA Kuongeza Elimu Kuhusu Kodi Ya Majengo

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya majengo na kuishauri kuongeza elimu zaidi juu ya umuhimu wa kodi hiyo.


Aidha,Akizungumza ofisini kwake wakati timu ya maofisa wa TRA kutoka mkoani Simiyu na Makao Makuu Dar es Salaam walipomtembelea kwa ajili ya kumpa taarifa ya semina za wafanyabiashara zilizofanyika mkoani humo, Mtaka amesema licha ya kazi kubwa ya uhamasishaji wa kodi ya majengo inayofanyika, bado kuna baadhi ya maeneo ambapo wananchi hawajapata elimu ya kutosha kuhusu kodi hiyo wahakikishe wanatoa elimu hiyo.

“TRA mnajitahidi sana kuhamasisha kodi ya majengo lakini bado kuna maeneo mengi elimu hii haijafika kama inavyotakiwa hivyo tumieni kila njia ya mawasiliano kuhakikisha kuwa elimu ya kodi ya majengo inawafikia wananchi wote,” alisema Mtaka.

Hata hivyo, Mtaka ameongeza kuwa, kuna haja ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kufungua ofisi katika baadhi ya wilaya ambazo hakuna ofisi za TRA ili kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo. 

“Kuna baadhi ya wilaya hazina ofisi za TRA hapa nchini, kwa mfano mkoani kwangu Simiyu, kuna Wilaya ya Itilima na Busega ambazo hazina ofisi za TRA na hivyo wananchi wa wilaya hizi hulazimika kufuata huduma kwenye ofisi za TRA zilizoko makao makuu ya mkoa,” alifafanua Mtaka.

Naye, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Diana Masalla amemshukuru Mkuu wa Mkoa huo kwa ushirikiano anaoutoa kwa TRA katika kutekeleza majukumu yake ya ukusanyaji mapato mkoani humo.

Hata hivyo,Mamlaka ya Mapato Tanzania ndio yenye jukumu la kukusanya kodi ya majengo kisheria na viwango vya kodi hiyo ni shilingi 10,000 kwa nyumba za kawaida, shilingi 20,000 kwa ghorofa zima katika Halmashauri za Wilaya na shilingi 50,000 kwa kila sakafu ya ghorofa katika Majiji, Miji na Manispaa.

No comments

Powered by Blogger.