Serikali Yaweka Kipaumbele Katika Kuimarisha Michezo Kwenye Mitaala Ya Mafunzo Ya Ualimu
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele katika kuimarisha michezo kama eneo muhimu la mtaala wa mafunzo ya ualimu kutokana na ukweli kwamba michezo inaimarisha stadi za kujifunza, nidhamu na ni ajira pia.
Hayo yamesemwa Mkoani Mtwara na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga Mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara (UMISAVUTA).
Amesema pamoja na kuwepo kwa mchepuo wa michezo katika baadhi ya vyuo vya Ualimu ni vizuri Vyuo hivyo kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu wakaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ufundishaji na ujifunzaji wa michezo na sanaa unalenga kuwawezesha vijana kufanya vizuri katika eneo hilo kwa maendeleo yao na Taifa.
Ametaja Vyuo ambavyo kwa sasa vinatoa mchepuo wa michezo kuwa ni Chuo cha Ualimu Tarime, Butiama, Butiama Mtwara Kawaida na Ilonga na kwamba Wizara itahakikisha kuwa michezo inaimarishwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini.
Naibu Waziri Ole Nasha amevitaka vyuo vya ualimu kuhakikisha vinaendeleza michezo chuoni kutokana na faida zitokanazo na michezo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahitimu wa mafunzo ya ualimu wanapata mafunzo ambayo wakihitimu wanakwenda kuwa walimu mahiri wa michezo katika shule za msingi na sekondari ambapo ndipo wanamichezo na wasanii wanaandaliwa.
“Nimefarijika kuona mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu imerudi tena baada ya kutokuwepo kwa miaka 20 iliyopita, hatuna budi kuwekeza katika michezo kwa sababu ni fursa za kuweza kusaidia kukua kiuchumi. Nchi nyingi duniani michezo imekuwa sehemu kubwa ya kusaidia kukua kiuchumi,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambae pia ni Afisa Elimu Mkoa Germina Mng’aho amesema kufanyika kwa michezo hiyo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inataka kuwepo kwa mashindano ya michezo kwa shule na vyuo ili kuwezesha kuinua vipaji ambavyo vitaleta mafanikio katika michezo ya kitaifa na kimataifa.
Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agusta Lupokela amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua faida zinazopatikana katika michezo ikiwemo stadi za kujifunza na kuamua kurejesha mashindano ya michezo kwenye Vyuo vya Ualimu.
Akitoa taarifa ya mashindano hayo kwa Naibu Waziri Mwenyekiti wa UMISAVUTA Taifa Agustine Sahili amesema kuwa michezo hiyo imeendeshwa kulingna na taratibu za michezo na matokeo yameamuliwa kwa weledi na haki katika kupata washindi.
Sahili ameiomba Wizara kuimarisha kozi ya michezo na fani mbalimbali za ndani katika vyuo vya ualimu ili wataalamu waweze kupatikana shuleni ambako ndiko chimbuko halisi la vipaji linapatikana lakini pia kuwajengea uwezo wasimamizi na waamuzi wa michezo kwa kuendesha kozi fupi na ndefu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Pia ameiomba Wizara kuongeza wakufunzi wa michezo na Sanaa vyuoni kwani kwa sasa vyuo vingi havina wakufunzi wa aina hiyo hali inayodunisha uendeshaji wa michezo na ukuzaji wa vipaji kwa vijana chuoni ambapo pia inasababisha shule za msingi na sekondari kukosa walimu mahiri katika michezo na Sanaa.
Nae Mshiriki wa Mashindano ya Michezo na Sanaa Albert Thomas kutoka Kanda ya Ziwa ameishukuru Serikali kwa kurejesha mashindano ya UMISAVUTA kwani inawasaidia kujenga afya na akili lakini pia inawasaidia kuwa na uelewa wa masula ya michezo na kutoa elimu ya michezo kwa wanafunzi ambao watakwenda kuwafundisha baada ya kumaliza masomo yao. Ameiomba Serikali kuendeleza vipaji vya wanamichezo wanaoshinda katika mashindano ya ngazi ya shule na vyuo ili visiishie kwenye ngazi ya kitaifa bali katika ngazi za kimataifa.
Ufungaji wa mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa vyuo vya ualimu yaliyoanza Oktoba 25, 2019 na kuhitimishwa Oktoba 31, 2019 yamepambwa na mechi kati ya Kanda ya ziwa na Kanda ya kusini ambapo Kanda ya ziwa wameibuka kidedea baada ya kuwafunga Kanda ya Kusini goli moja kwa sifuri.
No comments
Post a Comment