Header Ads

Header ADS

Bodi ya nishati vijijini(REB)yajadili kufuta Mkataba wa Mkandarasi wa REA.

    Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeweka mjadala wa kutaka kufuta mkataba mmoja wapo wa mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Mtwara na sehemu ya Mkoa wa Tanga, ambaye ni muunganiko (JV) wa kampuni za Radi Services Ltd, Njarita Contractors Ltd & Aguila Contractors Ltd.
    Ambapo suala hilo limewekwa wazi  mbele ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi hiyo, Mhandisi Styden Rwebangila, mkoani Mtwara.
   Rwebangila alikuwa akitoa majumuisho ya ziara ambayo yeyé na wajumbe wa Kamati husika walifanya mkoani Mtwara kwa muda wa siku mbili, wakiiwakilisha Bodi nzima, ambayo ililenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
   Alisema, Kamati imeamua kuweka kusudio hilo kutokana na sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni kusuasua kwa utekelezaji wa mradi katika maeneo ambayo mkandarasi husika amepewa kimkataba kuyafanyia kazi huku akiwa haoneshi dhamira ya kufanya mabadiliko chanya.
   Alisema, Kamati imeamua kuweka kusudio hilo kutokana na sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni kusuasua kwa utekelezaji wa mradi katika maeneo ambayo mkandarasi husika amepewa kimkataba kuyafanyia kazi huku akiwa haoneshi dhamira ya kufanya mabadiliko chanya.















    Alisema, kitendo cha Mkandarasi kutoonekana kwenye kikao, kinadhihirisha kuwa hatoi kipaumbele kwa mradi huo muhimu na wa kimkakati kwa serikali.

Akieleza zaidi kuhusu kusudio la kufuta mkataba, Rwebangila alieleza kuwa, Kamati yake imetoa maagizo kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Huduma za Ufundi, Mhandisi Jones Olotu, kufanya tathmini kati ya Mtwara na sehemu ya Tanga, ambako mkandarasi husika anatekeleza mradi, wapi panasuasua zaidi ili mkataba wake ufutwe.

Alisema, Kamati yake itawasilisha mapendekezo ya kusudio hilo katika kikao cha Bodi na endapo litapitishwa, utafanyika utaratibu mwingine wa kukamilisha mradi katika eneo husika ambapo alisema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linaweza kupewa kazi hiyo.

Aliongeza kuwa, kusudio la kufuta mkataba katika eneo mojawapo kati ya mawili aliyonayo mkandarasi, haimaanishi eneo atakalokuwa amebaki nalo litatelekezwa bali Bodi na Serikali kwa ujumla itamfuatilia kwa ukaribu mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kikamilifu mahali patakapokuwa pamesalia ili wananchi wapate huduma ya umeme kama ilivyokusudiwa.

Akijibu moja ya maswali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu nini Bodi imejifunza katika ziara hiyo; Mwenyekiti Rwebangila alisema “Bado tuna safari ndefu ya kuwalea wakandarasi wazawa.”

Akifafanua, alisema, serikali imekuwa na nia njema kuhakikisha inawapatia kazi wakandarasi wazawa lakini asilimia kubwa, hususan wale walioungana, wanaiangusha serikali kwani hawatekelezi miradi kwa viwango na kasi inayotakiwa.

Alitoa wito kwa wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kukumbuka kuwa wamepewa dhamana hiyo na serikali ili wananchi wa vijijini wapate umeme na hakuna kitakachobadilisha dhamira hiyo njema ya serikali, bali hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wale wanaokuwa vikwazo ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi (REA), Mhandisi Jones Olotu, alisema Ofisi yake imepokea maelekezo yote ya Bodi na itayatekeleza kikamilifu.

Aidha, akizungumzia suala la utaratibu wa kisheria kuhusu kufuta mkataba wa mkandarasi, Mhandisi Olotu alieleza kuwa hatua mbalimbali zimefuatwa ikiwemo TANESCO kumwandikia barua za maonyo muhusika pamoja na kukaa naye vikao mbalimbali ili ajirekebishe lakini kwa bahati mbaya hajaonesha dhamira ya kubadilika.

“Miradi hii ni ya kimkakati kwa serikali na sheria iko wazi. Hata hizo barua za maonyo alizoandikiwa ni moja ya vigezo vinavyoweza kutumika kufuta mkataba,” alifafanua.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wake, Meneja Mradi wa Kampuni hiyo ya Ukandarasi, Mhandisi Jofrey Luzinge, alisema atafikisha maagizo yote yaliyotolewa na Bodi kwa Uongozi na kwamba anaamini bado wanayo nafasi ya kujirekebisha na kukamilisha kazi husika kwa wakati na viwango, endapo watapewa ridhaa hiyo.

Kamati hiyo imekamilisha awamu ya kwanza ya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hususan katika maeneo ambako miradi inasuasua. Maeneo yaliyotembelewa ni Tabora, Kigoma, Mwanza, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Mtwara.
  Aidha,Kwa mujibu wa Mwenyekiti, Kamati hiyo itakuwa na awamu nyingine ya ziara ambapo maeneo mengine mbalimbali nchini yatatembelewa.

No comments

Powered by Blogger.