Header Ads

Header ADS

Milioni 31 zaahidiwa kutolewa kwaajili ya ukamilishaji wa Bweni la Misungwi Sekondari.

     Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameahidi kutoa shilingi milioni 31 kwa shule ya Sekondari Misungwi ili kukamilisha ujenzi wa bweni linalojengwa na shule hiyo.
   Ndalichako ametoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki alipofika shuleni hapo kukagua miundombinu ya shule hiyo ambapo  Serikali imejenga madarasa mapya, maabara na Bweni yaliyowezesha wanafunzi kuongeza ari ya kusoma na kupelekea shule hiyo Kuongoza katika mtihani wa kidato cha sita Mkoani  Mwanza na kuongeza idadi ya  wanafunzi.

   Ndalichako akiwa shuleni hapo amesema amefurahishwa kuona uongozi wa shule hiyo  umekuwa ukitumia fedha vizuri na kuweka akiba  kidogokidogo kwa miaka mitatu ambapo kupitia  kupitia akiba hiyo wamepata fedha  ambazo zimewawezesha kuanza ujenzi wa bweni jipya.
  "Nimefurahishwa  na mpango wa shule wa kuhifadhi fedha kidogo kidogo mpaka wamepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni la watoto wa kike jitihada hizi ni lazima ziungwe mkono nami nikiwa waziri mwenye dhamana ya elimu natoa ahadi ya kuleta fedha za kumalizia huu ujenzi " Alisema waziri Ndalichako.
  Aidha,Profesa Ndalichako amesema kuwa pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi pia atahakikisha samani za bweni hilo jipya zinanunuliwa  ili  likamilike na kutumika kwa wakati maalumu.
  Pia, Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi katika shule hiyo kuzingatia masomo na kutojiingiza katika mambo ambayo yatawakatisha masomo yao na mwisho kutofikia malengo yao.
  Hata hivyo,Mkuu wa Shule ya sekondari Misungwi Mwanani Asembandwa amemshukuru Waziri wa Elimu kwa kutambua jitihada za shule za kuweka fedha kidogokidogo kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana
   Pia,Asembandwa amesema  kuwa shule hiyo imefanikiwa kuwekeza fedha kidogo kidogo mpaka ikafanikiwa kupata shilingi  milioni 44  ambazo zimetumika kuanzisha ujenzi wa bweni la wasichana ambalo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa wakati mmoja.
   "Kukamilika kwa bweni hili kutasaidia kutatua changamoto ya sehemu ya kulala kwa wanafunzi wetu kufuatia ongezeko  pamoja na kuongeza wigo wa kutoa elimu katika mazingira bora" Mkuu huyo wa Shule ameeleza.
    Pia, Mwanafunzi wa shule hiyo Zamda Robert amemshukuru Waziri kwa kutoa ahadi hiyo ambayo inakwenda kupunguza changamoto ya malazi shuleni hapo ambapo wameahidi kuongeza bidii ya kusoma na hivyo kuongeza ufaulu wake.

No comments

Powered by Blogger.