Header Ads

Header ADS

Serikali imewataka Makamanda wa polisi kusimamia kampeni za Wagombea wa Serikali za mitaa .

   Kangi Lugola,Waziri wa mambo ya ndani ya nchi amewataka makamanda wa polisi nchini kusimamia kampeni zilizoanza za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwalinda wagombea wa vyama vya siasa ambavyo vilitangaza kujitoa, pamoja na kuwashughulikiwa bila huruma watu waliopanga kufanya vurugu. 
  Hivyo Waziri huyo amesema ana taarifa za kutosha kuhusu baadhi ya watu waliopanga kufanya vurugu wakati wa kampeni kwa lengo la kuvuruga uchaguzi huo, aliwataka makamanda hao kuwasaka kila kona, kuwakamata watu hao ambao wana nia mbaya ya kuvuruga uchaguzi huo.


  Lugola ameyazungumza hayo wakati wa maadhimisha miaka 15 ya Kumbukizi ya kifo cha Baba yake mzazi, James Ndege Lugola, tukio lililofanyika Kijijini kwa Waziri huyo, Nyamitwebili, Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, leo, na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wakiwemo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa kutoka Mkoani humo na nje ya Mkoa.
  “Nawataka mtende haki katika usimamizi wa uchaguzi huu, lakini wapo baadhi ya watu ambao wamepanga kufanya vurugu, watu hao msicheke nao, watu hao washughulikieni bila huruma, na badala ya kuwamwagia maji ya kuwasha, sasa watumbukizeni ndani ya tenki la maji hayo ili waweze kuwashwa zaidi, hatutaki vurugu, tunataka amani na utulivu ndani ya nchi yetu,” alisema Lugola.
   Hivyo, Kwa upande wa vyama vya siasa vilivyojitoa kushiriki uchaguzi huo, Lugola alisema wagombea wapo ambao wamekataa agizo hilo la vyama vyao, hivyo wameamua kushiriki uchaguzi huo wakigombea nafasi walizoziomba, hivyo wanapaswa kulindwa kwa nguvu zote kwani ni haki yao kugombea.
  “Wameweka mpira kwapani, lakini wachezaji wapo uwanjani bado wanataka kucheza,bado wanaenda uwanjani kuwapiga wachezaji hao wasiweze kucheze, bado wanataka kuwapiga waamuzi wasiweze kutoa pointi tatu muhimu kwa timu ambayo imeendelea kucheza,  hao muwashughulikie kiisawasawa,” al Lugola alisema.
  Aliongeza kuwa, agizo alilolitoa Waziri Mkuu la kuwataka Watanzania kushirikia uchaguzi huo kwa amani wakati alitoa hotuba yake Bungeni, hivyo Wizara yake inamhakikishia italinda amani hiyo katika kila mikutano ya hadhara, pamoja na kuwathibiti watakaofanya vurugu.
  Pia, Waziri Lugola aliwataka wananchi kwenda kusikiliza sera za wagombea wao kuanzia mwanzo wa kampeni mpaka utakapokamilika, na pia wapige kura kwa amani bila ya kuwa na wasiwasi wowote, kwasababu Jeshi la Polisi limeapa kuwanga kuwalinda wananchi hao pamoja na mali zao.
  Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Makamanda wa Polisi Mikoa ya Mara na Kanda Maalum Tarime/Rorya ambapo waliahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Waziri Lugola kwa kuimarisha amani katika Mikoa yao.
 Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Sillah, alieleza ameyapokea maelezo ya Waziri huyo, na askari wake wamejipanga vizuri kulinda amani mkoani humo, na aliwataka wananchi kuacha kuvuruga amani.
  “Tumepokea maelekezo na tutayafanyia kazi, sisi Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri kulinda amani katika kampeni zitakazoanza kesho, wakati wa kupiga kura na kipindi cha  kuhesabu kura, tunawataka wananchi kutokuvuruga amani, na watakaofanya vurugu tutawashughulikia,” alieleza Sillah.
  Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alimshukuru Waziri huyo kwa ushirikiano wake wa kumpigia sim umara kwa mara akitaka kujua hali ya amani ndani ya kanda hiyo, ushirikiano huo umemsaidia kufanya kazi kwa kasi zaidi.
  “Waziri Lugola wewe ni mtendaji Mkuu wa Wizara yetu, lakini umetutumia kadi ya mwaliko mpaka tumefika hapa, ulikua na haki ya kutuambia waambie hao waje, umetupa heshima kubwa sana, mheshimiwa waziri mara nyingi sana umenipigia simu kunionya na kunielekeza, mara nyingi unaponipa kazi nikikuambia unaniamini, haiwezekani mkoa wa mara ambao wewe ni mzaliwa wa mkoa huu ni mlezi kiusalama, itakua aibu sana kutokee uhalifu mkubwa katika mkoa unaotoka wewe, ni aibu sana,”  Mwaibambe alieleza.
 Aidha, Kwa upande wake, Mkazi wa Kijiji hicho, Lucas Magesa Masinde, akimshukuru Waziri Lugola kwa kuwaalika wananchi hao, na pia kuwahakikishia usalama kipindi hiki cha uchaguzi, hivyo ameahidi kujitokeza bila woga kusikiliza kampeni za wagombea, kupiga kura na atakapotangazwa mshindi.

No comments

Powered by Blogger.