Header Ads

Header ADS

Waziri Mwakyembe atoa agizo Vyombo vya habari kulinda usalama wa Wanahabari.

     Dk. Harrison Mwakyembe ambae ni  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,amesema kuwa Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa kuhakikisha kuwa maisha ya wanahabari yapo salama,ambapo amesema kauli hiyo wakati akifungua kongamano la wanahabari kuhusu usalama, ikiwa ni sehemu ya siku ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanahabari.
   Aidha,Alisema katika kongamano hilo linalofanyika mjini hapa kuwa Usalama kwa mwanahabari unaanzia katika chumba cha habari na chombo chake cha habari.
Alisema mwanahabari anapoandika habari, ipo haja ya kuelewa kama familia yake iko vyema kiasi gani.
     “Unapokaa unaandika stori, watoto kama wanaumwa … “ alisema Waziri Mwakyembe na kuongeza kuwa  ni lazima chombo cha habari kuhakikisha kwamba huyu hana shida katika kazi zake.
Aidha alisema usalama huo maana yake ni mshahara wake na bima kwani hivyo viwili ndivyo vinamfanya awe na uhakika wa maisha yake na usalama wake na familia yake.















   Alisema kukosekana kwa mishahara au mishahara kuwa midogo kunadhalilisha taaluma kwani mwandishi huyo anaweza kukengeuka katika kazi zake kwa sababu za bahasha.
Alisema mwanahabari anapolazimika kumuomba mtoa habari fedha ni kudhalilisha taaluma.
“Mwanhabaari ambaye anaenda kazini bila uhakika wa mshahara ni tatizo. Mtu aandika habari za uchunguzi akiwa karibu ya kukamilisha ,…. Anampa kitu anachukua”  alisema Mwakyembe na kuongeza kuwa akishachukua habari ile iliyokuwa na manufaa makubwa kwa wananchi inakufa.
Waziri Mwakyembe alisema mazingira hayo ya kukosekana kwa bima na mshahara kunatengeneza mazingira ya wanahabari kutokuwa wazuri katika taaluma yao.
“Mwanahabari wa leo lazima awekewe bima. Anayebisha ni nani. Si lazima kutokee machafuko. Mwanahabari huyu anaweza kusubiri kitu katika mvua mpaka akipate halafu anapata nyumonia” alisema na kuongeza kuwa haiwezekani kusibiri michango wakati wa kufa.
Aidha akizungumzia sheria ya habari, alisema kwamba sheria hiyo ipo kumlinda mwanahabari na kwamba zaidi ya mambo manne yanatajwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo mpaka sasa hayajafanywa.
Alisema sheria hiyo haiwezi kuchambuliwa bila mambo manne yanayohusiana na sheria hiyo kutekelezwa.

Mambo hayo ni pamoja na uwapo wa Baraza Huru la Vyombo vya Habari, Baraza la Ithibati ambalo linatambua nani mwanahabari na kupanga kanuni, Kuanzishwa kwa kamati ya mamalalamiko ambayo ina maamuzi sawa na mahakama na kuwapo kwa mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.
Alisema sheria imelenga taaluma ya habari kujiendesha yenyewe na bado mambo hayajakaa sawa na ikiendelea hivi lazima serikali ichukue hatua.
Aidha alisema haiwezekani kubadilishwa kwa kiwango cha elimu kwa kuwa waandishi wa habari ni walimu wa taifa na haikubaliki kuwa na walimu wasiojua kufundisha.
Alitaka kukomeshwa kwa tabia ya vyombo vya habari kutafuta makanjanja kwa kuwa wanawalipa fedha kidogo.
    Mwandishi wa habari mwandamizi Jesse Kwayu akitoa shukurani kwenye ufunguzi huo aliitahadharisha jamii ya wanahabari kuhusu uzingatiaji wa maadili ya taifa hili.
Pia alitioa tafakari ya mahusiano kati ya wanahabari na serikali na kusema ni vyema washirkiane kumtumikia mwananchi lakini wasiwe na urafiki wa mashaka kama kuwapo kwa shamba na mwanakondooo wakinywa maji katika kisima kimoja.
Aidha alitaka usimamizi wa sheria wa umakini na usiodhuru watu wengine au kuwakandamiza.















   Kila Novemba 2 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanahabari ikiwa ni kuikumbusha dunia haki ya upatikanaji wa habari na kuwalinda watoaji habari.
Sherehe hizo ambazo huadhimishwa kimataifa zina lengo la kukumbusha uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari huru kwa kuwa ni muhimu katika kukuza uelewa na kuboresha demokrasi, ikiwa ni sehemu moja muhimu ya utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia.
Katika miaka ya karibuni, kumekuwepo na matukio yanayotishia usalama wa wanahabari na vyombo vya habari na hivyo kutishia utendaji kazi wao.
Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba wanahabari na vyombo vya habari na wale wanaosaidia wanahabari kufanyakazi zao wamekuwa wakitishiwa maisha, kushambuliwa, kufungwa, kutishiwa kukamatwa, kunyimwa haki za kukusanya habari na kushindwa kupatiwa ufumbuzi wa matukio mabaya yanayofanywa dhidi yao na watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO)  Audrey Azoulay katika kipindi cha muongo mmoja (miaka 10) wanahabari 851 wameuawa na kwa mwaka huu pekee (2019) wameuawa wanahabari 44.
Pia alisema katika taarifa yake ya siku hii ya kupinga ukatili dhidi ya wanahabari, kwamba katika kila mashauri 10 ya ukatili, mashauri 9 yanayogusa wanahabari hayajapatiwa ufumbuzi.
Alisema wakati wanahabari wanahenyeka katika matukio hayo ya dhuluma jamii pia hulipa gharama kubwa kwa mateso yao. Bila kuwa na uwezo wa kulinda wanahabari hali ya jamii kuendelea kukosa taarifa muhimu zitakazowezesha kufanya maamuzi yenye  weledi hutibuka.
Bila waandishi wa habari kuwa na nafasi ya kufanyakazi zao kwa usalama, ipo hatari dunia kukosa taarifa na hivyo kuleta sintofahamu katika mambo muhimu.
Katika siku hii ni vyema dunia ikasimama na kuungana na wanahabari kwa ukweli na haki.
Kutokana na mazingira yalivyo duniani kote, UNESCO Tanzania imeandaa kongamano la wiki moja kuhusu uangalizi na utoaji taarifa juu ya usalama wa wanahabari Tanzania.
Kongamano hilo linalofanyika huku kauli mbiu ikiwa kuuweka ukweli hai (Keep Truith Alive) limelenga kuwezesha jamii na taifa kwa ujumla kuwa na uwezo wa kuhakikisha usalama wa wanahabari wake kwa kuzingatia malengo ya maendeleo endelevu ya dunia 16.10.1 na 10.2 yanayohusiana na usalama wa wanahabari na upatikanaji wa habari.
Kongamano hilo pia litatumika kuangalia hatua zilizofikiwa hadi sasa nchini Tanzania kufuatia maazimio ya mwaka jana; ikiwamo kujua na kuangalia na kuupitisha mfumo wa kuangalia usalama wa wanahabari nchini unaozingatia makubaliano ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Kongamano hilo la wanahabari limewezeshwa na UNESCO kutokana na ufadhili wa Shirika la misaada la Sweden (SIDA) katika mchango wake kwenye Mpango wa Kimataifa wa Maendeleo ya Mawasiliano (IPDC) kwenye akaunti maalumu ya mradi wa uimarishaji wa mchango wa vyombo vya habari kwa maendeleo endelevu.
Mradi huo umelenga kuimarisha maarifa na uwezo wa kuangalia usalama wa wanahabari Tanzania ikiwamo ufuatiliaji wa kisheria wa matishio yaliyoripotiwa.
Washiriki wa kongamano hilo ni pamoja na Idara ya Habari (MAELEZO), Tume ya haki za binadamu na utawala bora (CHRAGG), Jeshi la Polisi Tanzania, Jukwaa la Wahariri (TEF), Baraza la Habari (MCT), MISA Tanzania, Chama cha wanahabari wanawake Tanzania (Tamwa), Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Muungano wa Radio za jamii (TADIO), Uhuru Media (public media), Mwananchi Communications (private media), Millard Ayo (online media), Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) na maofisa habari wa mikoa.

No comments

Powered by Blogger.