Bodi Ya Mikopo Yatangaza orodha mpya ya wanafunzi 698 waliofanikiwa kupata mikopo katika dirisha la rufaa
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya majina 698 ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupata mikopo katika dirisha la rufaa kufuatia kukosa au kupata kiwango kidogo cha mkopo katika awamu nne zilizopita.
Wanafunzi hao 698 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 2.46 bilioni na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo hadi sasa kufikia 49,485. Taarifa ya kina kuhusu utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 itatolewa wiki ijayo baada ya uchambuzi wa mwisho kukamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema leo (Jumamosi, Desemba 7, 2019) jijini Dar es salaam kuwa taarifa zaidi kuhusu viwango walivopangiwa zinapatikana katika akaunti zao binafsi walizotumia kuomba mkopo – Student’s Individual Permanent Account (SIPA) kupitia https://olas.heslb.go.tz
“Tumeshaweka taarifa za hawa wanafunzi katika mfumo na hivyo kila mmoja anatakiwa aingie katika akaunti yake ya SIPA ambapo ataona taarifa zake ambazo pia zinatumwa vyuoni,” amesema Badru.
Kwa mujibu wa Badru, HESLB imeboresha mifumo yake na hivyo wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza walioomba mikopo wanaweza kuona taarifa zao kutoka popote walipo kwa kutumia simu zenye mtandao wa intaneti (simu janja).
Taarifa hii pia inapatikana kwenye mitandao ya kijamii na tovuti ya HESLB ambayo ni www.heslb.go.tz
Imetolewa na:
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
No comments
Post a Comment