Header Ads

Header ADS

Jaji Mkuu atoa ushauri kwa Mawakili wapya

       Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amewashauri Mawakili wapya kutumia elimu ya sheria kibiashara ili kuweza kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira katika sekta hiyo.
 Kauli hiyo ameitoa katika mahafali ya 61 ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya 558 yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sheria kwa Vitendo (School of Law)  jijini Dar es Salaam.
     Ambapo alisema sekta hiyo, katika karne ya 21 inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni shinikizo la kiuchumi, kijamii na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
    Alisema uzoefu wa huko Marekani katika kukabiliana na changamoto ya  Mawakili kukosa ajira ni kuwapatia elimu maalum ya biashara, na mbinu za kufanya biashara.
“Mawakili lazima watambue Makampuni yao ya Uwakili (Law Firms) ni biashara kama zilivyo biashara zingine. Ujuzi wa biashara utamwezesha Wakili afahamu biashara ya Kampuni yake ya Uwakili. ujuzi wa biashara ni zana ya kuendeshea Kampuni yako ya Uwakili au biashara nyingine yoyote ile”, alisema Jaji Mkuu.

 Aidha, alisema kuwa ujuzi katika biashara utawaweka katika hali ya utayari wa kushidana katika soko la huduma ya uwakili katika dunia ambayo mipaka ya huduma hizo  na zinginezo zenye ushindani mkubwa.

Aliongeza kuwa changamoto ya Mawakili kukosa ajira za kudumu ipo katika  nchi nyingi kama  vile Australia, Marekani, na Kanada.

“Mawakili lazima mkubali ushindani kutoka nje ya Tanzania. Jengeni madaraja ya ushirikiano na Mawakili wenzenu vijana wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili mtafute biashara ndani na nje ya Tanzania”, alisisitiza.

Aliongeza kwamba mawakili hao, wanapaswa kujifunza lugha za kimataifa  kwa ufasaha mfano:- Kiingereza, Kifaransa na Kichina.

Naye Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onorius Njole amewashauri, kuwa kwenda kufanya kazi katika maeneo yaliyo mbali na miji mikubwa yakiwemo maeneo ya vijijini kwa kuwa yana uhitaji mkubwa wa huduma hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala aliwasii wafanye kazi za uwakili kwa bidii, weledi na kuzingatia maadili ili kuiwezesha Mahakama kutimiza jukumu la msingi la kutenda haki.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma hapa Tanzania inaonyesha kuwa ni idadi ndogo  ya wahitimu wa Sheria walioomba kujaza nafasi za kazi katika Utumishi wa Umma ndio walifanikiwa kupata ajira 2017/2018, ambapo  walioomba walikuwa 3,250 waliopata walikuwa 88 sawa na asilimia 2.7na mwaka  2018/22019 walioomba walikuwa 2,826 waliopata walikuwa 19 sawa na asilimia 0.6.

No comments

Powered by Blogger.