Header Ads

Header ADS

Serikali Kuanzisha Vituo Vya Malezi Ya Watoto Nchi Nzima

           Serikali imeanza mpango wa kuwa na vituo vya malezi kwa watoto nchini nzima ili kuhakikisha wanajamii wanayapa kipaumbele malezi na makuzi kwa watoto ili kuhakikisha kunakuwa na taifa madhubuti.
         Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Semina ya Mafunzo ya Elimu ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

      Dkt. Jingu amesema kuwa vituo hivyo vitaratibiwa na Serikali ila vitaendeshwa na kusimamiwa na wananchi katika maeneo yao na mpaka sasa kuna zaidi ya vituo 1500 nchi nzima na vingine vinaendelea kuanzishwa.

Ameongeza kuwa malezi ni msingi mkubwa katika kuhakikisha tunapata kizazi chenye maadili, uwajibikaji na uzalendo katika kizazi itakayosaidia kujenga taifa bora.

"Mafunzo haya ni muhimu na mmeamua suala sahihi, watoto wanahitaji malezi ya karibu na sio malezi tu bali wapate malezi sahihi" alisema Dkt. Jingu

Dkt. Jingu pia amewataka washiriki wanatumia stadi hiyo kuisaidia jamii na nchi kuweza kuwa na muelekeo mzuri kwa kuwa na vijana wazalendo wawajibikaji kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde amesema kuwa Wizara ya Elimu itahakikisha inashirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha  Elimu ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa watoto inatekelezwa.

Ameongeza kuwa Wizara ya Elimu imehakikisha kila Chuo cha Maendeleo ya wananchi kinakuwa na kituo cha kulea watoto ili kuhakikisha inawasaidia watoto.

Naye Mwakilishi wa washiriki ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mbinga Bw. Lotty Mwang'onda amesema kuwa mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuleta mabadiliko hasa katika jamii inayowazunguka katika vyuo vyao ili kuhakikisha malezi, maendeleo na makuzi yanazingatiwa katika ukuaji wa mtoto.

Ameongeza kuwa wao kama washiriki wameshukuru kwa uzoefu na kama wataalam wa wanaofanya kazi na jamii watashirikiana na jamii kuhakikisha elimu walioyoipata inawafikia jamii inayowazunguka.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Karibu Tanzania KTO Bw. Aidan Mchawa ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa ushirikiano wao na asasi za kiraia katika kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha program ya Malezi, maendeleo na makuzi ya awali ya mtoto inarudisha misingi ya malezi ya mtoto hasa wa kitanzania.

Naye mshiriki Bi. Felister Nanguka ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa elimu ya mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi katika jamii hasa vijijini na kuahidi kufanya kazi hiyo kwa nguvu zao kwa kukaza msuli ili kuhakikisha watoto wanapata malezi stahili.

Shirika la Karibu Tanzania KOT limeandaa mafunzo kwa wakufunzi kutoka vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu malezi, maendeleo na makuzi ya awali ili wakaitoe elimu hiyo kwa jamii inayowazunguka.
 

No comments

Powered by Blogger.