Header Ads

Header ADS

JAFO ATAKA WANAFUNZI KUTOZUIWA KUANDIKISHWA SABABU YA KUKOSA VYETI VYA KUZALIWA

       Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb) amesema ni marufuku mwanafunzi kuzuiliwa kuandikishwa darasa la kwanza kwa sababu ya kukosa cheti cha kuzaliwa.

Jafo ameyasema hayo wakati wa ziara yake Wilayani Bahi kukagua uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa shule za msingi pamoja na mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule za sekondari.

Amesema amepokea malalamiko kutoka baadhi ya maeneo kuwa wanafunzi wa darasa la kwanza hawaandikishi kama hawana vyeti vya kuzaliwa.


“Nimeona nitoe ufafanuzi kuhusu suala hili kuwa cheti cha kuzaliwa ni haki  ya kila mtoto lakini isimzuie mtoto huyo kuanza shule eti kwa sababu tu hajapata cheti hicho; Watoto wote wapokelewa, waandikishwe na waanze masomo huku wazazi wao wakiendelea na mchakato wa kuwatafutia vyeti hivyo.

Sitaki kusikia eneo lolote mtoto ameachwa kupokelewa na kuanza shule kwa sababu ya kukosa cheti cha kuzaliwa, mzazi ahakikishe ndani ya miezi minne amepata cheti hicho lakini mtoto huyo aanza masomo wakati masuala ya cheti yanaendea kushughulikiwa kwenye mamlaka husika," Amesema Jafo.

Akizungumza wakati akikagua mapokezi ya kidato cha kwanza amesema wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti katika muda uliopangwa na wapokelewe bila masharti ya kuleta unga, mahindi au maharage.

Pia Waziri Jafo amepongeza uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa umakini waliouonyesha katika zoezi zima za uandikishaji wa darasa la kwanza linaloendelea na maandalizi mazuri katika mapokezi ya kidato cha kwanza, halkadhalika katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Munkunda amesema katika Halmashauri ya Bahi walishafanya kampeni ya upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano hivyo watoto wengi wanaonza shule hivi sasa wanavyo vyeti hivyo na endapo mtoto yeyote atakua hajapa basi ataandikishwa shule ndipo mchakato kwa cheti utafuata.

Kwa upande wa mapokezi ya kidato cha kwanza amesema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Wilaya ya Bahi ni 2712 na changamoto iliyopo ni uhaba wa madawati ambayo wameshaanza kuitatua kwa kuchonga madawati yatakayokidhi idadi ya wanafunzi hao.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mkakatika John Laurent Josephat amesema shule yake ina malengo ya kaundikisha wanafunzi 180 na kwa siku ya kwanza tu shule ilivyofunguliwa wameandikisha wanafunzi 134.

“Wanafuzi wote walioletwa shuleni kwetu tumewaandikisha na endapo mtoto hana cheti cha kuzaliwa tulitumia kadi la Kliniki kupata taarifa sahihi za mtoto na hatujarudisha mwanafunzi hata mmoja wote wamewpokelewa na wameanza masomo” Amesema Mwl Josephat.

Ameongeza kuwa uandikishaji huu kwa siku ya kwanza tu ni zaidi ya aslimia 70 hivyo anategemea tutaandikisha zaidi ya malengo waliyojiwekea.

Shule ya msingi Mkakatika ni miongoni mwa shule bora katika Wilaya ya bahi na ndiyo iliyoongoza kwa kuwa shule ya kwanza kiwilaya katika matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2019

No comments

Powered by Blogger.