Mfanyabiashara Kutoka India Yuko Nchini Kuangalia Fursa Za Uwekezaji
Mfanyabiashara kutoka nchini India, Bw.Vivek Agarwala yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku saba kuanzia tarehe 6 hadi 12 Januari 2020. Bw. Agwarala ambaye amekuja kuangalia fursa za uwekezaji nchini, atafanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya CRDB, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na kutembelea maeneo kadhaa kwa lengo la kupata maelezo kuhusu taratibu na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Maeneo yatakayotembelewa na mfanyabiashara huyo ni Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) Dar es Salaam, Mkoa wa Simiyu ambapo ataangalia uwezekano wa kupata eneo la ekari elfu mbili (2,000) kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha mpunga na ujenzi wa kiwanda zao hilo. Bw. Agarwala atatembelea maghala ya pamba ili kujiridhisha kabla ya kununua kiasi cha robota laki moja (100,000) ambayo aliahidi kununua wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya CRDB mwezi Desemba 2019.
Bw. Agarwala pia atatembelea machimbo ya Tanzanite, mkoani Manyara, Kiwanda cha Karatasi cha Mufindi kilichopo mkoani Iringa na kuangalia uzalishaji maparachichi ili kujenga kiwanda cha kusindika zao hilo kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.
Ujio wa mfanyabiashara huyo ni matokeo ya juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini India ambao uliratibu ziara ya kikazi iliyofanywa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji-Uendeshaji na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts iliyofanyika nchini India mwezi Desemba mwaka jana. Ziara hiyo ililenga kutafuta wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo soko la pamba nchini humo.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.
No comments
Post a Comment