Header Ads

Header ADS

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Tuhuma Zinazosambaa Mitandaoni Kwamba Wagonjwa Wengi Wanapoteza Maisha Katika Hospitali Ya Taifa Muhimbili-mloganzila.

                 Kumekuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii  ambazo bila kuchanganua zinatuhumu kwamba Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inasababisha vifo kwa wagonjwa. 
    Uongozi wa hospitali unapenda kuwahakikishia Umma wa Watanzania kwamba habari hizi si za kweli na hazitoi picha halisi ya huduma ambazo zinazotolewa hospitalini hapa.
  Takwimu tulizonazo zinaonyesha kwamba wagonjwa wanaotibiwa MNH- Mloganzila wameongezeka katika makundi yote.  Wagonjwa wa nje wameongezeka kutoka 17,115 katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 kufikia wagonjwa 25,493 katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia 48.8.   
Aidha, wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa wameongezeka kutoka 1,459 katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia wagonjwa 2,795 katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia 91.6. 
 
Wakati huo huo idadi ya vifo (mortality rate) ikipungua kutoka asilimia 14.9 iliyokuwepo katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia asilimia 10.4 katika kipindi cha Julai-Septemba 2019.
 
Aidha, takwimu za MNH-Upanga zinaonyesha kwamba katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba 2018 wagonjwa waliolazwa walikua ni 12,375 ambapo kulitokea vifo 1,000 (mortality rate) ambayo ni asilimia 8.1. 

Vilevile katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2019 MNH Upanga ililaza wagonjwa 17,230 na kati ya hao vifo vilikua 1,673 ambayo ni asilimia 9.7(mortality rate).
 
Hivyo basi takwimu kati ya MNH-Mloganzila na MNH-Upanga za asilimia ya wagonjwa waliofariki hazitofautiani sana ambapo MNH-Upanga ni asilimia 9.7 wakati MNH-Mloganzila ni asilimia 10.4 katika robo ya Julai – Septemba, 2019.  

Hatua hii inaonyesha juhudi ambazo zinafanyika za kuboresha utoaji wa huduma katika MNH- Mloganzila zinazaa matunda.
 
Moja ya sababu ambazo imeelezwa na mtoa taarifa kwamba Madaktari wanaotoa huduma MNH-Mloganzila ni wanafunzi waliopo katika majaribio si za kweli, hivyo tungependa kufafanua kwamba Hospitali ya MNH-Mloganzila ina Madaktari Bingwa 52, Madaktari wa kawaida 50 na kwa sasa ina Madaktari tarajali 53.
 
Licha ya Madaktari Bingwa hawa walioajiriwa MNH-Mloganzila kutoa huduma lakini pia wanashirikiana na Madaktari Bingwa kutoka MNH-Upanga katika kutoa huduma hapa MNH-Mloganzila, vilevile hospitali hii ina madaktari wawili waliobobea wenye hadhi ya Profesa kutoka Korea nao wapo wanatoa huduma.
 
Hivyo sio kweli kwamba madaktari ambao wapo mafunzoni wanafanyakazi bila usimamizi kwani hospitali imeweka utaratibu wa kila mgonjwa anayefika kupata huduma anaonwa na Daktari Bingwa kwa ajili ya maamuzi.
 
Wakati uongozi wa hospitali ukifanyia kazi tuhuma na malalamiko yaliyotolewa juu ya utoaji huduma katika taarifa hii, tunapenda kuutarifu Umma kwamba tangu MNH ipewe dhamana ya kusimamia hospitali hii, tumejielekeza katika kutatua changamoto zilizokuwepo katika utoaji huduma na kwa kiasi kikubwa imeonyesha mafanikio ambayo yanaonyesha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa na pia kuna ushuhuda wa wagonjwa ambao wametibiwa na kuridhika na utoaji wa huduma zetu.
 
Tunawahakikishia Watanzania kwamba huduma zinazotolewa katika Hospitali ya MNH-Mloganzila zimeboreshwa na tunawakaribisha Watanzania wenye jukumu la kuelimisha jamii waje kuzungumza na wataalam na waone jinsi huduma zinavyotolewa ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa jamii.

     Imetolewa na
    Prof. Lawrence M. Museru
    Mkurugenzi Mtendaji,
   MNH-Mloganzila.

No comments

Powered by Blogger.