Meza 100 kutolewa katika shule za sekondari wilayani wanging'ombe
jumla ya meza 100 na viti vimekabidhiwa kwa shule za sekondari wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe ikiwemo shule ya Thomasi Nyimbo,Philipo Mangula, Igwachanya na Wanike huku kila shule ikipokea meza 25 na viti vyake ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya halmashauri hiyo kuwa na akiba ya meza kwa ajili ya shule zote 16 wilayani hapo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo kwa walimu wakuu wa shule hizo, mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe Ally Kasinge amesema,madawati yametolewa na halmashauri kutokana na mapato ya ndani, lengo kuhakikisha shule zote za sekondari zinapa madawati ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati.
“Niwatoe hofu kwamba utaratibu huu unaendelea,bado ofisi ya mkurugenzi ina deni tena la kukamilisha agizo hili la mkuu wa wilaya madawati mia mbili,lakini wadau wengine wa maendeleo wanaendelea kututengenezea madawati,hatimaye kwa mwaka huu 2020 shule zetu zote za za serikali 16 za sekondari zitapata madawati 25 kila shule”alisema Ally Kasinge
Aidha Kasinge amesema mpaka sasa kiwango cha kuripoti kwa wanafunzi kidato cha kwanza kinaridhisha kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2020 wameshajiunga na ametoa wito kwa wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto wao shuleni kuwapeleka kabla ya tarehe 14 ya mwezi wa pili mwaka huu.
“Halmashauri ilikuwa imepangiwa jumla ya watoto 3431 kwa ajili ya kidato cha kwanza kwa mwaka 2020 na tangu shule za sekondari zifunguliwe tarehe 6 januari 2020 hadi sasa wanafunzi waliolipoti ni 2987 ambao hawajaripoti ni 444 tu,na hili nalo nitoe wiki mbili maafisa tarafa simamieni”alisema tena Kasinge
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Anton Mawata amemshukuru mkuu wa wilaya kwa jitahada za kuhakikisha asilimia 87 ya wanafunzi wameripoti shuleni nakuanza masomo yao ikiwa ni tofauti na miaka mingine ya nyuma.
“Mwaka huu hata mwezi haujaisha tumeshafika asilimia 87 kwa kweli inabidi tujipongeze sana jambo ambalo miaka mingine huwa tunakuta mwezi wa tatu au wanne ndio tunafika asilimia hiyo kwa kweli inatakiwa tujipongeze sana”alisema Anton Mawata
Baadhi ya walimu wa shule za sekondari ambao wamepokea madawati akiwemo kaimu mkuu wa shule ya Igwachanya Amelye Chatanda na shule ya Philipo Mangula Joseph Gobo wameishukuru serikali kwa kuwakabidhi madawati na kueleza kuwa kupitia madawati hayo kutasaidia kutatua changamoto ya miundombinu na itachochea ukuaji wa taaluma.
No comments
Post a Comment