TAKUKURU YAKAMILISHA UCHUNGUZI WA MAKUBALIANO YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI NA KAMPUNI YA ROM SOLUTIONS KWA ASILIMIA 99.9
TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
- TAKUKURU YAKAMILISHA UCHUNGUZI WA MAKUBALIANO YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI NA KAMPUNI YA ROM SOLUTIONS KWA ASILIMIA 99.9
Ndugu Waandishi wa Habari,
Tumewaita kwa mara nyingine tena kama ilivyo utaratibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU kwamba tunapokuwa na jambo la kuujulisha umma tunawaita na kuzungumza nanyi.
Tunaendelea kutoa shukrani zetu kwa namna mnavyoitikia wito wetu kila mara tunapowaita na jambo hili linaonesha ni kwa namna gani Vyombo vya Habari vimedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali za Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Nimewaita leo ili kupitia kwenu, tuujulishe umma juu ya kazi ya uchunguzi iliyofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU kuhusu MKATABA WA MAKUBALIANO (MoU) KATI YA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI NA KAMPUNI YA ROM SOLUTIONS Co. LTD ULIOHUSU UPATIKANAJI WA MKOPO WA EURO 408,416,288.16 (TAKRIBAN SHILINGI TRILLIONI 1 ZA KITANZANIA).
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kama mnakumbuka, Januari 23, 2020 (Takriban mwezi mmoja uliopita), Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo kwa TAKUKURU la kuanzisha uchunguzi kuhusu MKATABA WA MAKUBALIANO (MoU) iliyosainiwa kati ya JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI NA KAMPUNI YA ROM SOLUTIONS Co. LTD.
Sisi sote tunafahamu kuwa VITA dhidi ya ubadhirifu wa fedha, mali pamoja na rushwa ni moja ya kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Dkt John Pombe Joseph Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mara zote amekuwa akisisitiza uwazi na uwajibikaji kwa watumishi na Serikali kwa ujumla.
Kwa kutambua hilo, ndiyo maana TAKUKURU imekuwa ikiujulisha umma mafanikio ambayo TAKUKURU imeweza kuyafikia katika kufuatilia ubadhirifu wa fedha, mali pamoja na rushwa katika operesheni zake mbalimbali inazozifanya.
UCHUNGUZI ULIOFANYIKA:
Ndugu Waandishi wa Habari,
- Tuhuma hii inamhusisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi – Kangi Lugola, Aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji – Thobias Andengenye, pamoja na watumishi wengine wa umma wapatao 15.
- Uchunguzi huu ulihusu kusainiwa kwa Mkataba wa Ununuzi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni moja kinyume cha Sheria za nchi.
- Fedha iliyohusishwa katika tuhuma hii ni takriban Shilingi Trilioni 1 za kitanzania.
- Baada ya maelekezo ya Mhe. Rais, TAKUKURU ilianzisha uchunguzi mara moja kwa kukusanya vielelezo na kufanya mahojiano na watu mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Watumishi wa Serikali pamoja na makampuni husika katika MoU hiyo.
- Uchunguzi huu ulilenga kuthibitisha iwapo kuna uwezekano wa baadhi ya watumishi kufanya uzembe kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutozishauri Mamlaka zao kuhusu taratibu mbalimbali za usajili wa makampuni pamoja na uzingatiwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma?
- Je, kuna makosa ya kushawishi, Kuomba au Kupokea Rushwa kinyume Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
- Uchunguzi huu umelenga kuthibitisha iwapo waliosaini makubaliano hayo kwa niaba ya pande mbili husika walikuwa na uhalali wa kisheria wa kufanya hivyo.
- Je, Kampuni husika zina uhalali wa kisheria wa kuingia makubaliano yoyote ya kizabuni na taasisi za hapa nchini.
- Je kuna masuala ya ukwepaji wa Kodi halali ya Serikali au Ubadhilifu wa mali ya umma?
- Je kuna matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyotamakwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007?
Makosa hayo yote tuliyoyachunguza yanaangukia katika makosa ya uhujumu uchumi ambayo kisheria TAKUKURU haitakuwa na mamlaka ya kuyafikisha mahakamani. Kitakachofanyika ni kuwasilisha Jalada la Uchunguzi katika Ofisi ya Taifa ya Mashitaka ili kwa kibali chake watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani.
Tulipenda tuufahamishe umma kwamba tuko katika hatua ya mwisho ya kukamilisha uchunguzi huu ambapo baada ya wiki moja tutakuwa tayari kwa kukabidhi jalada hili katika Ofisi ya Taifa ya Mashitaka.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Tumesema kwamba Uchunguzi wetu umekamilika kwa asilimia 99.9 kwasababu Ushahidi muhimu dhidi ya tuhuma hii tayari umepatikana na kilichobaki ni taratibu za uwasilishaji wa jalada hili la uchunguzi katika Ofisi ya Taifa ya Mashitaka.
Ndugu Waandishi wa Habari,
KUIBUKA KWA MATAPELI
Kupitia hadhira hii ninapenda kuutahadharisha umma juu ya kuibuka kwa MATAPELI wachache ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa wakiwarubuni wananchi wakiwemo wafanya biashara pamoja na watumishi wa umma.
TAKUKURU imekuwa ikipokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wateja wetu kuhusu uwepo wa tabia ya baadhi ya watu wanaofanya UTAPELI kwa kujitambulisha kuwa wao ni Maafisa wa TAKUKURU.
Matapeli hawa wamekuwa wakiwaomba fedha baadhi ya wananchi kwa madai kuwa wanachunguzwa na TAKUKURU na kwamba wao wanaweza kuwasaidia ili kusitisha uchunguzi. Mbali na kuwatapeli watu binafsi, MATAPELI hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwapigia simu za vitisho na utapeli.
Kwa mara nyingine tena tunatoa onyo kwa MATAPELI HAO na tunawapongeza wale wote walioweza kubaini kuwa watu hawa ni MATAPELI na kutoa taarifa TAKUKURU mara moja.
Hata hivyo, tunaendelea kusisitiza kutokubali kutapeliwa kwani TAKUKURU ni chombo cha Serikali kinachotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zote za Serikali na shughuli zote za TAKUKURU hufanyika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo katika kila mkoa na kila wilaya nchi nzima.
Ndugu Waandishi wa Habari,
TAKUKURU inaendelea kuwasihi wananchi popote pale walipo, waendelee kutupatia taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili tuhakikishe kwamba hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wasiolitakia mema Taifa letu.
TAKUKURU imeendelea kuboresha miundombinu ya kuwawezesha wananchi kuwasiliana nasi na kutupatia taarifa ambapo pamoja na kuwa namba za simu ya Dharura 113 ambayo ni BURE – TAKUKURU imeanzisha TAKUKURU APPLICATION ambayo inamwezesha mwananchi kuwasilisha taarifa za wanaojihusisha na rushwa kupitia Simu ya kiganjani.
Kupitia TAKUKURU APPLICATION, Mwananchi anaweza kutuma Picha mnato za matukio; Anaweza kutuma sauti na pia anaweza kutuma ujumbe mfupi wa maneno.
Taarifa hizo zitakazotumwa zitapokelewa moja kwa moja TAKUKURU katika ofisi maalumu ambayo maafisa wake wanafanya kazi saa 24.
Mbali na kutumia njia hizo, Mwananchi anaweza kufika katika ofisi zetu zilizoko katika kila mkoa, kila Wilaya na hata katika Vituo Maalum ambavyo vina mkusanyiko wa shughuli nyingi za kuichumi.
Ndugu Watanzania wenzangu,
RUSHWA NI ADUI ANAYEWEZA KUTUCHELEWESHEA MAENDELEO AMBAYO RAIS WETU – MHE. DKT JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI – RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AMEKUWA AKIYAPIGANIA USIKU NA MCHANA.
TUUNGANE PAMOJA ILI KUUNGA MKONO JITIHADA HIZI ZA RAIS WETU. TULETEENI TAARIFA NASI TUTAZIFANYIA KAZI KWA WAKATI NA KUWAPA MREJESHO.
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.
IMETOLEWA NA:
BRIG. JEN. JOHN J. MBUNGO
KAIMU MKURUGENZI MKUU TAKUKURU
No comments
Post a Comment