Waziri Mkuu atoa Takwimu ya laini za simu zilizo sajiliwa kwa alama za vidole.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Februari 2, mwaka huu laini za simu milioni 31.4 kati ya laini za simu milioni 43.9 (sawa na asilimia 71.6) zilikuwa zimeshasajiliwa kwa alama za vidole.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 7, 2020) katika hotuba yake aliyoitoa wakati kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi 31, mwaka huu.
Ameeleza kuwa zoezi la usajili wa laini za simu ni endelevu na akatumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi ambao hawajasajili laini zao za simu na wale ambao wanaendelea na zoezi la kupata vitambulisho vya uraia na wamekwishapata namba za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wasajili laini zao za simu kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma za mawasiliano.
“Ninatoa wito kwa NIDA, isogeze huduma za kutoa namba za vitambulisho karibu na wananchi kwa kadiri inavyowezekana. Lengo ni kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi ili wapate kupata namba za vitambulisho na kuwawezesha kusajili laini zao za simu na vilevile, kupata Vitambulisho vya Taifa kwa matumizi mengine muhimu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya kwanza.
“Hadi kufikia tarehe 2 Februari, 2020, Tume ya Uchaguzi imekamilisha uandikishaji wa wapiga kura katika kanda ndogo 12 kati ya 14 zilizopangwa katika ratiba ya uboreshaji wa awamu ya kwanza,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri mkuu amesema kuwa kanda ndogo zilizokamilisha zoezi hilo zinahusisha mikoa 22 ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Simiyu, Mwanza, Geita na Shinyanga. Mingine ni Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Singida, Dodoma, Songwe, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Njombe, Lindi, Mtwara, Tanga, Morogoro (Ulanga DC na Malinyi DC) na Tanzania Zanzibar.
Amesema zoezi la uboreshaji kwenye kanda ndogo ya 13 inayohusisha mkoa wa Morogoro, lilianza Februari 3, 2020 na linatarajiwa kukamilika Februari 9, 2020.
“Uandikishaji wa wapiga kura ni wa siku saba kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga kura. Aidha, zoezi la uboreshaji linahusisha uandikishaji wa wapiga kura wapya ambao hawajahi kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura, urekebishaji wa taarifa za wapiga kura walioandikishwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa ikiwemo kufariki.
“Idadi ya wapiga kura walioandikishwa kuanzia kanda ndogo ya kwanza hadi ya 12 walikuwa 18,058,977. Jumla ya wapiga kura 2,012,212 wamejitokeza kuboresha taarifa zao sawa na asilimia 11.14 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12,” amesema.
Amesema idadi ya wapiga kura wapya walioandikishwa katika kanda ndogo zote 12 ni 5,666,343 ambayo ni sawa na asilimia 31.38 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12. “Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 14.38 la makadirio ya awali (asilimia 17). Vilevile, idadi ya wapiga kura walioondolewa kwa kupoteza sifa ni 14,894 ambayo ni sawa na asilimia 0.08 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12.
Hata hivyo,Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuihamasisha Tume ya Uchaguzi iharakishe zoezi la uandikishaji. “Nitumie nafasi kutoa wito kwa Tume iongeze kasi ya uandikishaji. Pia, natoa rai kwa wananchi watumie haki yao hiyo ya kikatiba na wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao na kujiandikisha upya kwa wale wenye umri wa miaka 18 au watakaofikisha umri huo ifikapo Oktoba, 2020,” ameeleza.
No comments
Post a Comment