WHO yasitisha majaribio ya dawa ya Hydroxychloroquine
Majaribio yanayofanyiwa dawa ya ugonjwa wa malaria Hydroxychloroquine ili kuona iwapo inaweza kutibu virusi vya corona yamesitishwa kutokana na hofu ya usalama wake, shirika la afya duniani WHO limesema.
Vipimo vilivyokuwa vikifanywa katika mataifa kadhaa vimesitishwa kwa muda kama hatua ya kuchukua tahadhari, lilisema shirika hilo siku ya Jumatatu.
Hatua hiyo inajiri baada ya utafiti wa tiba uliofanyika hivi karibuni kusema kwamba dawa hiyo inaweza kuongeza hatari ya mgonjwa kufariki kutokana na virusi hivyo.
Rais Donald Trump amesema kuwa anatumia dawa hiyo kuzuia virusi hivyo.
Rais huyo wa Marekani ameikuza dawa hiyo ya malaria, kinyume na ushauri wa kimatibabu na onyo kutoka kwa maafisa wa Afya kwamba inaweza kusababisha tatizo la moyo.
Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins vifo vilivyotokana na corona vimefikia 98,218.
Wiki iliopita, utafiti uliofanywa na jarida la tiba duniani Lancet ulibaini kwamba hakuna faida yoyote kwa kutumia dawa ya Hydroxychloroquine na kwamba utumizi wake unaweza kuongeza idadi ya vifo miongoni mwa wagonjwa hospitalini walio na maambukizi ya corona.
Hydrochloroquine ni dawa salama ya kutibu ugonjwa wa malaria, baridi yabisi na Lupus, lakini hakuna majaribio yoyote ambayo yamependekeza matumizi yake kutibu Covid-19.
Watafiti wanasemaa kwamba wagonjwa wa Covid-19 hawafai kutumia hydroxychloroquine.
Shirika la Afya duniani linafanyia majaribio dawa kadhaa kuona iwapo zinaweza kutibu ugonjwa huo mbali na kuripoti kwamba baadhi ya watu binafsi wamekuwa wakitumia dawa hiyo na hivyobasi kujisababishia madhara makubwa.
No comments
Post a Comment