Rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera ameapa kudumisha mshikamano katika taifa hilo la kusini mwa Afrika. Chakwera aliapishwa Jumapili kuwa rais mpya wa Malawi baada ya kumshinda rais aliyekuwa madarakani, Peter Mutharika, aliyekuwa akitafuta muhula wa pili katika uchaguzi uliopingwa mahakamani. Chakwera, ambaye ni mchungaji wa kanisa, alitangazwa mshindi baada ya kujinyakulia asilimia 59 ya kura, kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa siku ya Jumamosi. Malawi linakuwa taifa la pili la kusini mwa Jangwa la Sahara kufuta matokeo ya urais mahakamani likitanguliwa na Kenya mwaka 2017. Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake, Chakwera ameapa kurejesha imani katika serikali inayowahudumia na kuwapigania wanachi. Rais huyo mpya anakiongoza chama kikongwe cha Malawi Congress Party (MCP), ambacho kiliwahi kutawala kati ya mwaka 1964 na 1994.
No comments
Post a Comment