WHO yapongeza matokeo ya utafiti wa Dexamethasona
Shirika la Afya Duniani (WHO) limefurahishwa na matokeo ya awali ya najaribio ya dawa ya kutibu corona Uingereza yanayoonesha kwamba dawa ya dexamethasone, inaweza kuokoa maisha ya watu walio mahututi wanaougua ugonjwa wa Covid-19.
Kwa wagonjwa wanaotumia mashine za kupumua, dawa hiyo ilionesha kwamba imepunguza idadi ya vifo kwa theluthi moja, na kwa wagonjwa wanaohitaji hewa ya oksijeni, idadi ya vifo ilipungua kwa humusi au moja ya tano kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na WHO.
Hata hivyo, faida ama uzuri wa dawa hiyo kulijitokeza kwa wagonjwa wanaoumwa sana kwasababu ya virusi vya corona wala sio kwa wenye athari za wastani za ugonjwa huo.
"Hii ndio dawa ya kwanza kupunguza idadi ya vifo kwa wagonjwa wa virusi vya corona wanaohitaji oksijeni au walio kwenye mashine za kupumua," amesema Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.
"Hii ni habari njema na ninapongeza serikali ya Uingereza, Chuo Kikuu cha Oxford, na hospitali nyingi na wagonjwa Uingereza ambao wamechangia katika utafiti huu wa kisayansi ambao ni mwokozi wa maisha."
Dexamethasone ni dawa ambayo imekuwa ikitumiwa tangu 1960 kupunguza uvimbe katika hali tofauti kama vile ugonjwa wa saratani, yabisi kavu na kadhalika.
Watafiti walishirikishana maoni yao ya awali kuhusu matokeo ya majaribio ya dawa hiyo na WHO, huku wakitarajia utafiti wa kina wa data siku za hivi karibuni.
Dawa ya bei rahisi inayopatikana kwa urahisi Dexamethasone inaweza kusaidia maisha ya wagonjwa wa virusi vya corona waliopo katika hali mahututi.
Wataalam wa Uingereza wanasema kwamba tiba hiyo yenye steroid ni hatua kubwa iliopigwa katika kukabiliana na virusi hivyo hatari.
Inapunguza hatari ya mtu kufariki kwa thuluthi moja miongoni mwa wagonjwa walio katika mashine za kuwasaidia kupumua.
No comments
Post a Comment