Rais wa Malawi afuta baraza la Mawasiri kwa tuhuma za ufisadi
Rais Lazarus Chakwera wa Malawi amechukua uamuzi wa aina yake baada ya kuwafuta kazi mawaziri wote wa baraza lake la mawaziri kutokana na madai ya ufisadi yanayotolewa dhidi ya baadhi ya mawaziri
Katika hotuba kwa taifa kwa njia ya televisheni, Rais Chakwera ameapa kukabiliana na aina zote za ukiukaji wa sheria unaofanywa na maafisa wa serikali. Rais wa Malawi amesema kwamba atatangaza baraza jipya katika muda wa siku mbili zijazo.
Waziri wa kazi anashutumiwa kwa kutumia vibaya pesa zilizo tengwa kukabiliana na janga la virusi vya Corona, huku Waziri wa Nishati akituhumiwa kuingia mikataba ya kijanja kuhusu mafuta. Mawaziri wote waliotajwa wamekana madai hayo.
Mawaziri watatu wanakabiliwa na mashtaka mahakamani, akiwemo Waziri wa Ardhi aliyekamatwa mwezi uliopita kwa madai ya kupokea rushwa.
Makundi yenye nguvu na ushawishi sana katika makanisa ya Malawi yalimueleza wiki iliyopita kwamba hakuwa akichukua hatua za kutosha kupambana na ufisadi.
Lazarus Chakwera aliyekuwa kiongozi wa upinzani Juni mwaka 2020 aliapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, baada ya kushinda uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali, ambao uliitishwa tena baada ya matokeo ya uchaguzi wa awali kubatilishwa.
Ushindi huo wa Chakwera ni mabadiliko makubwa ya kuchukua madaraka kutoka mikononi mwa Peter Mutharika aliyekuwa akishikilia kiti cha urais, ambaye ushindi aliopata katika uchaguzi wa mwezi Mei 2019 ulibatilishwa na Mahakama ya Katiba ya Malawi kutokana na madai ya udanganyifu.
No comments
Post a Comment