Chanjo ya Malaria imesaidia kupunguza maambukizi Kenya
Kila mzazi anataka wanawe wawe na afya nzuri pasina maambukizi au kuumwa. Eneo la kanda ya Ziwa nchini Kenya lina mandhari ya kuvutia ila amani hiyo hutatizwa na maambukizi ya malaria kwa kiasi kikubwa.
Tathmini ya Malaria nchini Kenya imeyatenga maeneo ya Siaya,Kisumu, Migori,Homa bay,Vihiga,Bungoma na Busia kuwa yale yanayotatizwa zaidi na malaria kwenye eneo la kanda ya Ziwa.Ya pwani ni pamoja na Mombasa, Kilifi, Kwale,Lamu na Taita Taveta.Kutokana na tathmini hiyo, serikali ilizindua mwaka 2019 chanjo ya Malaria mahsusi kwa watoto wadogo. Ugonjwa wa malaria ni moja ya vyanzo vya maafa kwa watoto wadogo hasa walio na umri wa chini ya miaka 5.
Mtoto wa kwanza
Elian ndiye mtoto wa kwanza kuwahi kuchanjwa malaria Kenya wakati ilipozinduliwa mwaka 2019.Kufikia sasa bado hajaambukizwa wala kuugua malaria.Mamake Elian aitwaye Noreen anasema kuwa,”amefurahi kuwa mwanawe na wengine wananufaika na chanjo hiyo mpya iliyo na uwezo wa kuzipunguza athari za Malaria kwenye eneo hilo la kanda ya ziwa.”
Chanjo ya malaria inatolewa kwa dozi nne pindi mtoto anapotimiza miezi 6 hadi 24.Inatolewa wakati mmoja na chanjo nyengine za utotoni wanapotimiza miezi 6,7,9 na 24.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watoto wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo ya malaria.Vita dhidi ya malaria vimeimarishwa na chanjo hii mpya ya RTS,S na shirika la afya ulimwenguni WHO limeidhinisha na kupendekeza matumizi yake kwa watoto.Hata hivyo utafiti unaendelea na chanjo mpya imeanza kufanyiwa kazi eneo la Kilifi la pwani ya Kenya.Dr Adam Haji wa WHO anaelezea kuwa,”Kuna chanjo nyengine ya R21 ambayo ni kama RTS,S.Utafiti uliofanywa Burkina Faso ulionyesha kuwa ina nguvu kuliko RTS,S lakini ilitumiwa katika mazingira ya malaria ya msimu.Kenya inafanya utafiti kwa sasa na tunarajia matokeo kuanzia mwezi wa sita mwaka huu,”anasisitiza.
Kina mama hushauriwa kuwalaza watoto chini ya vyandarua vya mbu vilivyotiwa dawa, kuhakikisha nyasi ndefu nje ya nyumba zinakatwa na kuzuwia maji kutuama karibu na makaazi kadhalika matumizi ya dawa ya kunyunyiza majumbani.Chanjo hii mpya itaimarisha mapambano hayo.Ili chanjo iwe madhubuti , ni muhimu kwa watoto kupokea dozi zote nne.Kulingana na shirika la afya ulimwenguni WHO, changamoto kuu ni kuwa baadhi ya wazazi hawajauona umuhimu wa kuwarejesha watoto kupokea dozi ya nne ya chanjo hasa waliotimiza miezi 24 kwa madai kuwa ni wakubwa.
Mwezi wa nne mwaka huu Jumuiya ya Afrika Mashariki ilizindua mkakati wa pamoja wa kupambana na malaria.Ijapokuwa hatua zimepigwa katika mapambano dhidi ya malaria,maambukizi yanaripotiwa kuongezeka kwa 12% kwasababu ya janga la COVID 19.Rais Uhuru Kenyatta ndiye mwenyekiti wa muungano wa viongozi wa Afrika unaopambana na Malaria,ALMA.Pindi baada ya kuteuliwa kuwa kiongozi wa muungano huo hadi mwishoni mwa 2022, Rais Uhuru Kenyatta alisistiza kuwa,”Tunapouanza muongo wa kuitokomeza Malaria, najitolea kuhakikisha kuwa tunaiongeza kasi ya mapambano ili ugonjwa huo uzikwe kwenye kaburi la sahau,”aliweka bayana.
Gharama za chanjo
Mpango mzima wa kugawa chanjo ya Malaria unafadhiliwa na washirika wa kimataifa mfano muungano wa kusambaza chanjo wa GAVI na shirika la PATH.Kwa Kenya, chanjo hiyo inatolewa bure hadi mwishoni mwa 2023 kwa ufadhili wa GSK,shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto-UNICEF,shirika la utafiti na uvumbuzi wa nyenzo za teknolojia ya afya -PATH na WHO ndiyo inayoratibu mpango mzima.
Mbinu za kupambana na malaria zinazopendekezwa na shirika la afya ulimwenguni WHO zimeleta tija katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Njia hizo zinajumuisha hatua mujarab za kuzuwia mbu kuzaana na kuwauma wanadamu pamoja na matumizi ya dawa za mchanganyiko za kutibu Malaria.
Malaria husababishwa na mbu wa kike aina ya anopheles aliyeambukizwa vimelea vya plasmodium.Ishara zake ni pamoja na ongezeko la joto mwilini,maumivu ya viungo,uchovu, kutapika au hata kifo inapokuwa kali.
No comments
Post a Comment