Amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 26, 2022) wakati akijibu maswali ya wabunge waliyomuuliza katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo. 

Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na wawekezaji wanalipwa fidia.

”Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna madai yametolewa na hasa kama uthamini umefanyika basi thamani ya ile ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya kupisha shughuli nyingine ni lazima fidia ilipwe ili haki itendeke,” ameeleza Waziri Mkuu.

Akijibu Swali ya Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupima maeneo ya Miji, Manispaa na Jiji, Waziri Mkuu amesema kuwa mpango huo ni endelevu wenye lengo la kupima maeneo yote nchini ili kubainisha huduma zote zinazotakiwa kutumika katika ardhi hiyo.

 “Tunataka watumie hati hizi kama mtaji wa kukopea kwenye taasisi zetu za fedha, lengo ni kila Mtanzania anufaike na ardhi iliyopo, hivyo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iendelee kukamilisha zoezi hili, hii itawasaidia hata wawekezaji kutambua maeneo ya uwekezaji,” amesema Majaliwa