Header Ads

Header ADS

NAIBU SPIKA: Zifungieni Hospital zinazoghushi


MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeagizwa kuzifungia hospitali zote zinazobainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu ili liwe funzo kwa hospitali nyingine na kulinda uhai wa Mfuko.




Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Spika wa Bunge Mhe. Mussa Zungu wakati akifunga semina kati ya Wabunge na Wizara ya Afya, semina iliyolenga kutoa uelewa wa masuala ya Bima ya Afya kwa wote.

Hili suala la udanganyifu ni kubwa na linaweza kuua Mfuko, hospitali zinazojihusisha na kughushi madai zifungieni ili ziwe mifano na wengine nao waache,” aliagiza.



Kabla ya agizo hilo, Wabunge waliochangia mjadala uliohusu hali halisi ya uendeshaji wa shughuli za NHIF, walilaani vikali hospitali kujihusisha na udanganyifu wa kughushi madai hali inayosababisha madhara makubwa kwa NHIF.

Akichangia hoja hiyo Mbunge wa Sengerema Mhe. Khamis Tabasamu alisema kuwa baadhi ya hospitali zinawasainisha wagonjwa fomu ya NHIF kabla ya kumaliza mzunguko wa huduma za matibabu na badae kuingiza madai yasiyo halali hivyo kusababisha mzigo mkubwa wa malipo kwa NHIF.

Naye Mbunge wa Lulindi, Mhe. Issa Mchungahela alizitaka hospitali hususan za binfasi kufanya kazi zake za utoaji wa huduma kwa kuzingatia uzalendo na kuacha mara moja vitendo vya udanganyifu ambavyo aliviita ni sawa na uhujumu uchumi.

“Kumekuwa na ubadhirifu mkubwa sana hospitali za binafsi hasa wanapotibu mwanachama wa NHIF, wanamuandikia mwanachama vipimo vingi ambavyo hata havihitajiki na lengo ni kupata fedha kwa njia isiyo halali, mimi mwenyewe ni shahidi nilienda moja ya hospitali nikaandikiwa vipimo vingi ambavyo hata sikuvihitaji hivyo ni vyema kuwa wazalendo ili kulinda Mfuko,” alisema Mhe. Mchungahela.


Katika Mada yake Mkurugenzi wa NHIF, Bw. Bernard Konga alielezea namna ambavyo Mfuko umekuwa ukipambana na suala la udanganyifu ikiwemo kuwakamata wanaobainika na kuwafikisha katika Mamlaka husika na wengine kurejesha fedha ambazo walilipwa baada ya kubainika zilitokana na udanganyifu.

Pamoja na jitihada hizo, alisema Mfuko unaendelea na mbinu mbalimbali za kuhakikisha wote wanaojihusisha na udanganyifu wanabainishwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

No comments

Powered by Blogger.