Header Ads

Header ADS

Serikali imesema mradi mkubwa wa gesi umeiva

   Serikali ya Tanzania inatarajiwa kusaini makubaliano ya awali na kampuni za kimataifa za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta juu ya mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi asilia (LNG) utakaotekelezwa mkoani Lindi, kilomita 460 Kusini mwa jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Utiaji saini huo wa mradi wa LNG wenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 70 ($30 bilioni) uliwekwa bayana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati wa mazungumzo yake na Tido Mhando wa Azam TV.

‘Kuhusu mradi wa kuchakata gesi nadhani mwezi wa sita (Juni) tutasaini mkataba tutauza gesi ndani na nje ya nchi’ alisema Rais Samia wakati akizungumzia matumizi ya gesi katika masuala mbalimbali ikiwemo kuzalisha nishati ya umeme.
Rais Samia hakutaja tarehe kamili ya kutiliana saini makubaliano hayo ya awali ya ujenzi wa mtambo huo ambao umekuwa katika mipango ya serikali kwa takribani miaka kumi sasa. Pia hakubainisha kampuni zitakazohusika.
Wakati wa kuwasilisha bajeti ya wizara ya Nishati bungeni mapema mwaka 2021 aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati huo, Dkt. Medard Kalemani alisema mradi wa LNG ungeanza kutekelezwa 2022 na kukamilika mwaka 2028, kwa kuhusisha kampuni za kimataifa za mafuta zikishirikiana na shirika la maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).Alisema uwezo wa mtambo huo ulitarajiwa kuwa ni kuzalisha tani za ujazo milioni 10 za LNG kwa mwaka.
Mradi wa LNG ndiyo utakuwa mradi wa gharama kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Tanzania.
Shilingi trilioni 70 za utekelezaji mradi huo ni takriban mara mbili ya bajeti ya taifa ya Tanzania ambayo ni shilingi trilioni 40 kwa mwaka mmoja wa fedha.
LNG ni gesi iliyochakatwa na kuwekwa katika mfumo wa kimiminika huku ikiwa imesindikwa kwa zaidi ya mara 600 kutoka katika ukubwa wake wa asili na kuwa katika hali ya ubaridi mkali wa nyuzi joto hasi 162 ili kurahisisha utunzaji na usafirishaji wake.
Tanzania ina akiba ya gesi zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 katika mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara. Imekuwa ikitumia gesi kuzalisha umeme uliounganishwa katika gridi ya Taifa tangu mwaka 2004.
Kadhalika Baadhi ya viwanda na nyumba za kuishi jijini Dar es Salaam zimeunganishwa na mfumo wa gesi asilia.


No comments

Powered by Blogger.