Serikali yaombwa kuingilia kati suala la kijana aliyepigwa risasi na mlinzi kwenye mgodi wa EL HILAL
Kufuatia kifo cha Kijana
Hamisi Mayunga (19) mkazi wa kijiji cha Dulisi Kata ya Sekebugolo wilayani
Kishapu mkoani Shinyanga, ambaye amedaiwa kuuawa na mlinzi wa kampuni ya Sam
Security Emmanuel Chacha ndani ya mgodi wa madini ya Almasi El- Hilal, kwa
kupigwa Risasi kifuani na kufariki dunia papo hapo , wadau wa haki za binadamu
wameiomba serikali kulishughulikia tatizo hilo ili kukomesha matukio ya
kikatili kama hayo.
Kauli hiyo imetolewa
na Mtetezi wa Haki za Binadamu John Myola kutoka Shirika la AGAPE ambaye ameshiriki
mazishi ya kijana huyo ambapo amelaani tukio hilo na kuomba Rais Samia Suluhu
Hassan aingilie kati juu ya matukio ya mauaji ambayo yanaendelea ndani ya mgodi
huo wa El-Hilal juu ya walinzi ambao wanaulinda kwa kuendelea kukiuka haki za
binadamu na kupoteza maisha ya vijana.
Amesema tukio hilo
siyo la kwanza ambapo kuna vijana wengi wamepoteza maisha na wengine kupata
ulemavu kwa kuendelea kupigwa na walinzi wa mgodi huo, ambapo Machi 10 mwaka
huu kuna kijana mwingine mkazi wa kijiji cha Mwang’olo Cosmas Hamisi (25) naye
aliuawa kwa kupigwa Risasi.
Kwa upande wake diwani wa Sekebugolo Frednand Mpogomi, akizungumza kwenye
Mazishi hayo leo Mei 24, 2022, amesema kifo cha kijana huyo kimeumiza wananchi
na kuviomba vyombo vya dola vitende haki juu ya kifo hicho.
“Tunalaani tukio la kifo cha kijana huyu na kimeumiza sana wananchi na hata
wengine kuzirai na tumewakimbiza hospitali kupata matibabu na imani vyombo vya
dola vitatenda haki juu ya kifo hiki, kijana alikuwa mdogo sana na tumepoteza
nguvu ya Taifa,”anasema Mpongomi.
Naye Baba mzazi wa kijana huyo Mayunga Inegele, amesema mtoto wake hakustahili
kifo hicho cha kikatili na kubainisha kuwa kama ni kosa kuingia ndani ya Mgodi
huo wangewachukulia hatua kali za kisheria na siyo kumpiga Risasi huko ni
kukiuka haki za binadamu.
Kaka wa Marehemu Robert Mayunga (21) ambaye walikuwa na mdogo wake ndani ya
mgodi huo wa El-Hilal wakivua Samaki, anasimulia kuwa siku hiyo walikwenda
kuvua Samaki majira saa moja jioni na walitega mitego yao kwenye bwawa hilo na
ilipofika saa 4 wakaenda kuota moto kwenye kambi yao maeneo ya vichakani ndani
ya mgodi huo na wakapitiwa na usingizi.
Amesema wakati wakiwa wamelala ilipofika majira ya Saa 6 usiku ndipo
wakashtukia wamewekwa chini ya ulinzi, na walipoanza kukimbia ndipo
ikafyatuliwa Risasi.
“Baada ya Risasi kufyatuliwa
ilibidi nikimbilie ndani ya maji kwenye bwawa ambalo tunavua Samaki nikajificha
humo, na walinzi walianza kunisaka kwa kumulika Tochi wakanikosa, na walipoondoka
ndipo nikatoka na kukimbilia nyumbani, kumbe ile Risasi ilikuwa imempiga mdogo
wangu,”amesema Mayunga.
“Kwenye mgodi huu siyo mara ya kwanza
kuingia hua tunaingia mara kwa mara kuvua Samaki na walinzi wanatufahamu
kabisa, lakini tuna shangaa siku hiyo sijui walipatwa na nini na kuamua kumuua
mdogo wangu,”ameongeza.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP George Kyando,
alikiri kutokea mauaji ya kijana huyo Hamis Mayunga kwa tuhuma za kupigwa
Risasi na Mlinzi wa Kampuni ya Sam Security Emmanuel Chacha ambaye amekimbia
mara baada ya kutokea mauaji hayo.
Amesema Jeshi hilo linamsaka mlinzi huyo, pamoja kushikilia wenzake wanne kwa
ajili ya upelelezi zaidi, huku akionya walinzi wa makampuni binafsi wajiepushe
na matumzi holela ya silaha na kusababisha mauaji.
Kijana Hamisi Mayunga (19) aliuawa Mei 20 mwaka huu, wakati akiwa na
wenzake wanne pamoja na kaka yake Robert Mayunga (21) wakiwa ndani ya Mgodi wa
Almasi El-Hilali wakivua Samaki katika bwawa lililopo ndani ya mgodi huo, ndipo
walipokamatwa na walinzi na kupigwa risasi na mwili wake tayari umeshazikwa.
Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE John Myola akiaga Mwili wa marehemu Hamis Mayunga, akiwa na wananchi wa kijiji cha Dulisi nyumbani kwao na kijana huyo kwa ajili ya mazishi.
Mwili wa marehemu Hamisi Mayunga ukipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
Wananchi wakiwa msibani.
No comments
Post a Comment