Header Ads

Header ADS

Taasisi ya wanawake 100 ,000 yampongeza rais samia kwa ujasiri wa kipekee kuongeza mishahara, kudhibiti bei ya mafuta na the royal tour

 

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake 100,000 (kulia), Vicky Kamata akiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyatt jujini Dar es Salaam leo akipongeza ujasiri wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kuleta ahueni kwa Watanzania kufuatia ongezeko la bei za mafuta duniani. Kushoto ni Josephine Matiro, Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000.

Balozi wa Utalii Tanzania na Mkurugenzi wa Miradi, Taasisi ya Wanawake 100,000 (katikati), Nangasu Warema akiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mwenyekiti wa Wanawake 100,000 Vicky Kamata na kushoto ni Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000, Josephine Matiro. Viongozi hao wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushujaa wa kipekee katika kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa 23.3%, kuchukua hatua za dharura dhidi ya bei ya mafuta duniani na kutangaza utalii na uwekezaji Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour.
Mkurugenzi wa Haki za Wanawake, Wanawake 100,000 (katikati) Josephine Matiro akiongea na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Balozi wa Utalii Tanzania na Mkurugenzi wa Miradi, Taasisi ya Wanawake 100,000 Nangasu Warema, kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake 100,000 (kulia), Vicky Kamata.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanawake Laki Moja ‘Wanawake 100, 000’ imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri wa kipekee, ubunifu na uthubutu wake katika kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa 23.3% kwa watumishi wa umma, kuchukua hatua za dharura kudhibiti bei ya mafuta duniani na kutangaza utalii na uwekezaji Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 20,2022 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Laki Moja, Vicky Kamata amesema Taasisi yao inampongeza Rais Samia kwa uongozi wake wa kishujaa, kumtia moyo aendelee na jitihada zake na kumhakikishia kuwa Watanzania wapo pamoja naye bega kwa bega kukabiliana na changamoto za maendeleo nchini.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI WANAWAKE TANZANIA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UJASIRI WA KIPEKEE 

Dar es Salaam, Mei 20, 2022
 Ifuatayo ni taarifa kwa vyombo vya habari nchini Tanzania kutoka kwa taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanawake 100,000.

 Taasisi yetu inawakilisha wanawake zaidi ya 100,000 kutoka kila kona ya nchi yetu na pia tunasimama hapa kwa niaba ya Watanzania wote nchini wanaopenda maendeleo ya taifa letu. 

Ndugu wanahabari, leo tumewaita hapa kuzungumzia masuala matatu makuu ambayo kwa sasa yameibua mijadala mbalimbali kwenye jamii, hususan nyongeza ya kima cha chini cha mshahara cha asilimia 23.3% iliyotangazwa na serikali hivi karibuni, jitihada za serikali kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta duniani na uzinduzi wa makala maalumu ya The Royal Tour uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni Marekani na nchini Tanzania. 

Tungependa kuchukua fursa hii kutoa pongezi za dhati kwa Rais Samia kuonesha ujasiri wa kipekee, ubunifu na uthubutu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizotokea nchini na duniani kwa ujumla tangu achukue uongozi wa nchi mwezi Machi mwaka jana (2021).

 NYONGEZA YA MSHAHARA

 Mnamo tarehe 14 Mei 2022, taarifa iliyotolewa na Ikulu ilitangaza kuwa Rais Samoa ameridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara, ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3 na hivyo kuibua shangwe kubwa nchini.

 Ongezeko hili la mshahara ni kubwa kuwahi kutokea nchini kwa kipindi kirefu sana. Kwa miaka mingi sasa, wafanyakazi nchini wamekuwa na kilio cha kutoongezwa mshahara na kutopandishwa vyeo kwa watumishi wa umma. 

Vile vile, mifuko ya pensheni nchini ilikumbwa na uhaba mkubwa wa fedha na hata kushindwa kulipa mafao kwa wakati kutokana na serikali kuwa na malimbikizo makubwa ya michango ya penchent ya watumishi wa umma. 

Ndani ya mwaka mmoja tu, Rais Samia ameweza kuongeza mshahara kwa 23.3%, amepandisha watumishi wa umma madaraja na kulipa malimbikizo ya mchango wa pensheni za watumishi wa umma.

 Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi trilioni 9.7 katika mwaka wa fedha ujao wa 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishara ya watumishi wa umma.

 Hili ni ongezeko la Shilingi trilioni 1.59 ukilinganisha na bajeti ya 2021/22.

 Ongezeko la kima cha chini cha mishahara pamoja na kupandishwa kwa madaraja kwa watumishi wa umma, siyo jambo jema kwa watumishi wa umma pekee, bali taifa zima.

 Maelfu ya walimu, manesi, askari na watumishi wa kada nyingine wataongeza kipato chao na mafao yao kutokana na ongezeko hili.

 Utafiti wa wachumi huonesha pia kuwa ongezeko la mshahara huleta chachu kwenye jamii yote, huongeza pato la taifa la hukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

 UDHIBITI WA BEI YA MAFUTA NCHINI 

Kama mnavyofahamu, hivi karibuni nchi mbalimbali duniani zimekumbwa na msukosuko wa kupanda kwa bei za mafuta kutokana na vita inayoendelea sasa hivi nchini Ukraine. 

Tanzania siyo Kisiwa na yenyewe pia inakabiliana na changamoto zitokanazo na bei ya mafuta kupanda ghafla kwenye soko la dunia na hivyo kuleta athari katika mfumuko wa bei, gharama za uzalishaji kwenye uchumi na kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi mijini na vijijini.

 Kwa ujasiri wa kipekee, Rais Samia ametoa maelekezo kwa serikali yake kuchukua hatua za dharura kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta duniani kabla ya mwaka ujao wa fedha wa 2022/23.

No comments

Powered by Blogger.