Urusi yatoa onyo kali kwa Marekani
Balozi wa Russia mjini Washington ametoa onyo kali kwa Marekani kutokana na kuendelea kwake kupeleka silaha nchini Ukraine na kuashiria kuwa, kitendo cha Marekani cha kuipa silaha Ukraine ni sawa na kuiangamiza nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Anatoly Antonov ametoa onyo hilo kwa kitendo cha Marekani cha kuendelea kumimina silaha zake huko Ukraine na kusema kuwa, kuna hatari kitendo hicho cha Marekani kikasababisha vita makabiliano baina ya madola mawili makubwa ya nyuklia ambayo madhara yake kwa dunia hayatabiriki kabisa.Amesema, kitendo cha Marekani cha kupeleka silaha kubwa zaidi huko Ukraine kimeifikisha hali ya mambo katika mazingira ya tishio na kuna hatari ya dunia kukumbwa na maafa yasiyotabirika iwapo madola hayo mawili makubwa ya nyuklia yataanza kukabiliana.
Onyo hilo la Russia limekuja baada ya Rand Paul, seneta wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican kumlaumu Joe Biden kwa kuendelea kuipa Ukraine misaada ya kila namna ya kijeshi na kuonya kuwa, kitendo hicho kinahatarisha usalama wa kitaifa wa Marekani. Seneta huyo aliandika juzi katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, mimi nimekula kiapo cha kulinda katiba ya Marekani si katiba ya nchi nyingine yoyote.
Baraza la Wawakilishi la Marekani hivi karibuni limepasisha msaada wa takriban dola bilioni 40 kwa Ukraine na kupeleka muswada huo kwa Baraza la Sanate la nchi hiyo. Iwapo muswada huo utapasishwa na Baraza la Sanate, kitakachobakia ni kutiwa saini tu na Joe Biden ili uwe sheria.
Matumizi ya kiholela ya fedha za taifa huko Marekani yanafanyika katika hali ambayo, mgogoro wa kupanda bei ya mafuta unaendelea kuvunja rekodi nchini humo na hivi sasa bei ya bidhaa hiyo muhimu imevunja rekodi ya historia nzima ya Marekani.
No comments
Post a Comment