Uturuki imewazuia wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuanza mazungumzo kuhusu maombi yaliyowasilishwa na Finland na Sweden ya kujiunga muungano huo wa kijeshi. Duru za kidiplomasia zimeiambia DW kuwa mjumbe wa Ankara ndiye pekee aliyepinga uamuzi wa kuanzishwa mazungumzo hapo jana. 

Finland na Sweden zilikuwa zimewasilisha maombi yao ya kujiunga na NATO siku hiyo hiyo. Wanachama wa NATO wanatumai kuwa suala hilo litatatuliwa kupitia mazungumzo kati ya Uturuki, Sweden na Finland. 

Uwanachama wa NATO utafikisha mwisho miongo mingi ya Finland na Sweden kutogemea upande wowote kijeshi. Nchi hizo ziliamua kutuma ombi la uwanachama baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

Ombi lolote la kujiunga na NATO lazima liridhiwe na wanachama wote 30 wa muungano huo. Mchakato huo kawaida huchukua hadi mwaka mmoja. Hata hivyo, Finland na Sweden huenda zikawa wanachama wa NATO ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kama mchakato huo utaharakishwa.