Header Ads

Header ADS

Waziri wa Mambo ya Ndani , Hamad Masaun, Atoa siku saba kwa Jeshi la Polisi kuwakamata Panya road

 Jeshi la Polisi limepewa siku saba kuhakikisha linawakamata vijana maarufu kwa jina la ‘Panya Road’ waliohusika kujeruhi na kuiba katika maeneo mbalimbali jijini hapa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni wakati vikundi hivyo vikiendelea kuzua hofu kwa uhalifu, huku viongozi mbalimbali wakikemea hilo, huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala akitangaza kuanza kwa msako mkali kuanzia juzi.

Wiki iliyopita Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilitangaza kuwakamata vijana 10 wanaotuhumiwa kuhusika kuwajeruhi watu 19 maeneo ya Tabata na Chanika pamoja na kuwapora mali zao.
Hata hivyo, juzi kundi lingine lilivamia eneo la Mjimpya, Kunduchi na kujeruhi watu 19, pamoja na kupora pesa, simu, pombe na sigara katika maduka.
Akizungumza na wakazi wa Zingiziwa Chanika jana, Masauni alisema hategemei baada ya siku saba kuona watu wanajeruhiwa, vijana wote watakuwa wamekamatwa na kuchukuliwa hatua.
“Maelekezo kwa Jeshi la Polisi hawa wanapobipu basi wapigiwe, natoa siku saba kuhakikisha wote waliofanya matukio wanakamatwa. “Kazi kwako IGP Sirro, anzeni na hao wazee wananaowafuga, sitaki kukufundisha kazi lakini nataka kuona wananchi wakiwa salama,” alielekeza Masauni.
Akizungumzia watoto wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu, Masauni alisema jukumu la kwanza la kumlea mtoto ni la mzazi mwenyewe, hivyo kutoruhusu mtu kuhatarisha maisha ya mwingine.
“Simamieni watoto wenu wajiepushe na makundi ya hovyo, mtu hajui mtoto anapolala na anapokuja na kitu ahoji alipokipata.
“Lingine ni ushirikiano na vyombo vya dola, katika ulinzi maelekezo yangu kwa Jeshi la Polisi watoe ushirikiano kwa wananchi,” alisema.
IGP Sirro afedheheshwa, aomba radhi
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro alisema yanapotokea matukio kama hayo sehemu anayotokea IGP, ni kumdhalilisha.
Alisema Waziri na Rais wana mambo mengi ya kufanya, yanapotokea matukio kama hayo tena yanafanywa na watoto chini ya miaka 15 ni fedheha kwa Jeshi la Polisi.
“Nimeshiriki kumhoji kijana mmoja Unusi, anaeleza ni utoto tu, alisema huwa wanakutana kwenye pool table na kwenye uwanja wa mpira, kati ya vijana 31, waliokamatwa 10 ni wa Chanika na 21 ni kutoka Kariakoo na Mbagala,” alisema Sirro.
Alisema ipo shida moja ya ubinafsi kwa baadhi ya watu, kutotaka kushiriki katika ulinzi shirikishi. “Tukitegemea askari pekee hawatoshi, tujitoe na wenyewe kuongeza nguvu.”
Wananchi watoa ya moyoni
Mkazi wa Chanika, Majaliwa Rashid alisema mambo yote yanayotokea yanasababishwa na wazazi, kwani wanapowaambia kuhusu uhalifu wa watoto wao husema tukawafunge sisi.
“Wazazi wamekuwa wanawatetea watoto wao kwamba siyo wahalifu na wengine kukiri kuwa wanavuta bangi tu, bila kufanya uchunguzi na kujiridhisha, hii ndio shida kubwa tuliyonayo huku,” alisema Majaliwa.
Naye Mariam Hassan, mkazi wa Mtaa wa Gogo alisema wiki iliyopita alivamiwa na vijana na kuwajeruhi watoto wake watatu ambao hadi sasa ameshindwa kuwatibu kutokana na kukosa fedha.
Alisema walipopelekwa Hospitali ya Amana walipewa Rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) lakini alitakiwa kuwa na Sh 1.4 milioni ili kufanyiwa upasuaji.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Zingiziwa, Maige Suleman alisema wazazi katika malezi kuna sehemu wamelegalega, kwani unaweza kukuta watoto chini ya umri wa miaka 15 wapo kwenye makundi ya ajabu na wanapotaka kuwachukulia hatua huja juu.
ACT Wanena
Kwa upande wa Chama cha ACT Wazalendo, kimelaani vikali vitendo vinavyofanywa na makundi hayo ya vijana na kulitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kulinda usalama wa raia na mali zao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Kisekta Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarara Maharagande, vijana hao wamekuwa na desturi ya kuvamia nyumba moja baada ya nyingine na kutekeleza matukio hayo.
“Matukio hayo yamekuwa yakifanyika kati ya majira ya saa nne hadi saa tano, mpaka sasa zaidi ya watu 89 wamejeruhiwa kwa mtindo wa kuingia nyumba moja baada ya nyingine.
“Serikali ifuate mipango ya uchumi tunayoielekeza kila mara ili kuondoa ugumu wa maisha na kuzalisha ajira zitakazopunguza vijana wasiokuwa na kazi kama hawa wanaojikita kufanya uhalifu,” alisema.


No comments

Powered by Blogger.