Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amegundua udanganyifu wa kisomi uliofanywa na mkandarasi wa mradi ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi ikiwa ni miaka miwili kabla haujakamilika.

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) tangu Februari 2020, una kila dalili kwamba Watanzania hawatapata thamani ya fedha zao iwapo usimamizi hautaongezwa.

Ujenzi wake utakaogharimu Sh602.19 bilioni zinazojumuisha Sh592.61 bilioni za ujenzi wenyewe na Sh9.58 bilioni za usimamizi, umeanza kwa mwanzo mbaya kuanzia kwenye uzingatiaji wa kanuni za utekelezaji wake mpaka tathmini ya athari za mazingira.

Kwenye ukaguzi wake uliojikita kuangalia usimamizi wa ununuzi, usimamizi wa fedha, usimamizi wa mikataba, masuala ya kiufundi na masuala ya mazingira kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2019 hadi Januari 31, CAG amegundua udhaifu utakaolitia hasara Taifa.

Kila mradi wa ujenzi, lazima kuwe na mshauri elekezi atakayesimamia na kuelekeza mambo ya kiufundi yanayotakiwa kuzingatiwa lakini Katika mradi huu, mambo mawili yalifanywa ambayo yameshaisababishia Serikali hasara ya mabilioni.

Kamati ya tathmini ya zabuni iliorodhesha na kupendekeza majina sita ya wahandisi washauri kwa bodi ya zabuni ya Tanroads ili waidhinishwe, lakini bodi hiyo iliwaondoa wawili kati yao bila kueleza sababu za kufanya hivyo.

“Ukaguzi zaidi ulionyesha Tanroads ilimbadilisha mhandisi mshauri ambaye hakuwamo katika orodha iliyopendekezwa na kamati ya tathmini, matokeo yake iliwanyima haki wazabuni walioshiriki mchakato wa zabuni. Pia, imesababisha tathmini ya zabuni isiyo ya haki ambayo inaweza kusababisha kumpata mshauri asiye na uwezo au atakayetoa huduma kwa gharama kubwa,” amesema CAG Charles Kichere.

Ingawa watendaji walikuwa wanafahamu kuhusu daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 ambalo ni kiungo muhimu kati ya Mkoa wa Mwanza na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi, likijengwa kuanzia Februari 24 mwaka 2020 na kukamilika Februari 24 mwaka 2024, bado walichelewa kumteua mhandisi mshauri kusimamia ujenzi huo.

Ingawa mkataba wa kazi ulisainiwa Julai 29 mwaka 2019, wa mhandisi mshauri ulisainiwa Desemba 27 mwaka 2019, Ucheleweshaji huu wa miezi mitano uliruhusu shughuli za ujenzi kuanza bila usimamizi.

“Maofisa wa Tanroads waliohojiwa walibainisha kuwa kutokuwapo kwa mhandisi mshauri, kazi ya usimamizi ilifanywa na Tanroads yenyewe,Sababu za kuchelewa kumpata mshauri ilihusishwa na urefu wa taratibu zilizopo,” amesema Kichere.

Sio tu Tanroads ilichelewa kumteua mshauri elekezi, haikumlipa kwa wakati pia. Masharti ya mkataba yanataka mshauri alipwe asilimia 15 ya malipo ya awali ndani ya siku 30, lakini Tanroads ilichelewesha malipo haya kwa siku 154 kutoka Juni mosi 2020 utekelezaji ulipoanza.

Hata hivyo, CAG anasema “ucheleweshaji huu ulisababishwa na kuchelewa kutolewa fedha kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kwani zilitolewa Novemba 2020.”

Sio mshauri elekezi pekee aliyecheleweshewa malipo. CAG anasema hata ya mkandarasi pia yalichelewa na Serikali ikalazimika kulipa faini.

Mkataba unaitaka Tanroads kumlipa mkandarasi kiasi kilichothibitishwa na meneja wa mradi ndani ya siku 28 tangu tarehe ya kila cheti cha utekelezaji na akichelewa basi atalipa riba itakayokokotolewa kuanzia tarehe ambayo malipo yalipaswa kufanywa.

Kutokana na ucheleweshaji uliofanywa, CAG anasema mwajiri alitakiwa kulipa riba ya Sh1.64 bilioni, ila alimlipa kwanza Sh1.55 bilioni.

“Ucheleweshaji wa malipo kwa mkandarasi na mhandisi mshauri kulichangiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuchelewa kutoa fedha kwenda Tanroads. Kama ucheleweshaji huu hautashughulikiwa, tozo za riba kwa mkandarasi zitaongezeka na kusababisha ongezeko la gharama,” ametahadharisha Kichere.

Mkandarasi acheza na vipimo

Mkataba unataka mkandarasi ajenge ofisi ya mhandisi itakayokuwa na chumba cha mikutano na stoo mbili. Sakafu ya ukumbi wa mikutano ilipaswa kuwa na ukubwa wa mita za mraba 20, huku sakafu ya stoo ikitakiwa kuwa na ukubwa wa mita tano za mraba kila moja.

Ufuatiliaji wa ujenzi ulibaini mkandarasi alijenga chumba cha mkutano chenye mita za mraba 18.33 kinyume na mkataba, huku kila stoo ikiwa na ukubwa wa mita za mraba 3.87.

“Mahojiano na maofisa wa mhandisi mshauri msimamizi yalionyesha hali hii ilisababishwa na kutokuwa na usimamizi wa karibu wakati wa ujenzi wa vyumba hivyo, hali iliyosababisha vipimo kutokidhi vigezo vinavyohitajika,” amesema CAG.

Ingawa hakuona fedha zilizolipwa, ila CAG anasema kutokidhi vipimo kunaweza kusababisha malipo ya ziada kwa mkandarasi ikilinganishwa na kazi iliyofanyika.

Mkandarasi pia hakusambaza samani na vifaa vinavyohitajika katika ofisi ya mhandisi. Mkataba unamtaka mkandarasi kuweka madawati sita yenye droo mbili kila moja ila ameweka moja tu, kufunga makabati sita ya chuma ila kafunga moja na alitakiwa kufunga mapangaboi 10 ila amefunga manane tu.

Vilevile, ukaguzi ulibaini vipande 10 vya mbao za ukutani zenye urefu wa mita moja na upana wa mita moja viliwekwa badala ya vitengo 10 vyenye urefu wa mita 2.4 na upana wa mita 1.2.

“Sababu ya kutoa kiasi kidogo cha samani ni kukosekana kwa usimamizi wa karibu wa mhandisi mshauri msimamizi, jambo linaloweza kusababisha malipo yasiyo na tija,” ametahadharisha Kichere.

Mkataba pia unamtaka mkandarasi kufunga viyoyozi katika kila nyumba ya mhandisi. Alitakiwa kufunga viyoyozi vitatu katika kila nyumba ya daraja la II na kimoja katika kila makazi ya watu wengi.

Uhakiki uliofanywa ulibaini viyoyozi viwili vilifungwa katika nyumba ya daraja la II badala ya vitatu katika nyumba nne za daraja hilo. Mkandarasi pia hakufunga kiyoyozi chochote kwenye vitengo vinne vya makazi ya watu wengi.

“Mahojiano yaliyofanyika yalionyesha kushindwa kusimika viyoyozi vyote 16 kulingana na vipimo vilivyowekwa kulisababishwa na kutosimamiwa ipasavyo kwa mkataba, hali inayosababisha kukosekana kwa thamani ya fedha kwa kuwa mkandarasi alilipwa kwa vitu ambavyo havikutolewa,” amesema CAG Kichere.

Hata maabara ambako vipimo vya malighafi tofauti zinazotumika kujenga daraja hilo zinapimwa, mkandarasi hakupeleka vifaa vyote vinavyotakiwa.

Mkataba unataka maabara ya uhandisi kuwa na vifaa vya kupima udongo na changarawe, kokoto na zege, pamoja na ‘asphalt’ kwa ajili ya lami.

Hata hivyo, ukaguzi ulikuta hakuna vifaa 24 vya kupima asphalt kwa ajili ya lami, vifaa 15 vya kupima udongo na changarawe, pamoja na vifaa 12 kupima kokoto na zege. Vifaa vingine vingi havikuwepo katika maabara hiyo, ukiwamo mzani wa kielektroniki, kipima unyevu na cha kupima msongamano wa nyuklia.

Vifaa hivi havikuwepo, ingawa tayari mkandarasi alikuwa ameshalipwa Sh201.16 milioni kati ya Sh205.27 milioni zilizotengwa.

Hakuna tathmini ya mazingira

Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara zake za kilomita 1.66 lilianza kujengwa kabla ya kutathmini athari za mazingira.

Ujenzi wa mradi huo ulianza Februari 2020, lakini cheti cha tathmini ya mazingira kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kilitolewa Machi 2021, zaidi ya mwaka mmoja tangu utekelezaji ulipoanza.

“Hii inaonyesha mradi ulitekelezwa bila kufuata masharti maalumu yaliyobainishwa katika cheti cha tathmini ya athari za mazingira. Ni muhimu kutathmini athari za mazingira na jamii kabla ya kuanza kutekeleza mradi wowote wa ujenzi,” ameshauri CAG.

Tathmini iliyofanywa na taasisi ya Wajibu inayohamasisha masuala ya uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma kutokana na ripoti ya CAG kwa mwaka 2020/21 inaonyesha kuna harufu ya rushwa kwenye miradi na zabuni nyingi.

“Matumizi ya Sh3.365 trilioni yana viashiria vya rushwa. Miradi ya Sh20 bilioni kwenye halmashauri tofauti nchini haikufanyiwa tathmini ya athari za mazingira na CAG amebaini kuwapo kwa uchimbaji wa madini katika hifadhi ya Taifa,” alisema Jackson Mmari, ofisa wa Wajibu.

Serikali yafafanua

Kuhusu kukosekana kwa mshauri elekezi wakati mradi umeanza kutekelezwa, katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye alikuwa Ofisa Tawala wa Mkoa wa Mwanza wakati mradi huo unaanza, Emmanuel Tutuba alisema kulikuwa na mbadala.

“Nilikuwa RAS (katibu tawala wa mkoa) wa Mwanza na tuliwahi kuutembelea mradi huo mara mbili. Nafahamu wakaguzi wa Tanroads walikuwa wanasimamia,” alisema Tutuba.

Kuhusu mkandarasi kujenga miundombinu na kusambaza baadhi ya vifaa tofauti na makubaliano ya mkataba, Tutuba alisema “kuna wakati huwa kunakuwa na mabadiliko ya vipimo tofauti na mkataba ulivyotaka.”