Ahmed Ally: Tutafanya usajili mkubwa msimu ujao
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba Ahmed Ally amesema klabu hiyo imepanga kufanya usajili wa wachezaji wenye hadhi ya juu barani Afrika kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Simba SC msimu huu imeambulia patupu baada ya kuutema Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, hali ambayo imeufanya Uongozi wa klabu hiyo kuanza mikakati ya kukisuka upya kikosi chao.
Ahmed Ally amesema Simba SC imedhamiria kufanya usajili mkubwa msimu ujao, na wachezaji watakaopewa kipaumbele ni wale walioziwezesha klabu zao kufika hatua ya Robo Fainali katika michuano ya Kimataifa msimu huu.
Amesema mbali na kuwatazama wachezaji wa namna hiyo, pia Uongozi wa Simba SC, umedhamiria kuendelea na baadhi ya wachezaji waliopo kikosini kwa sasa, huku wengine wakitarajia kupewa mkono wa kwaheri.
“Simba SC kwa sasa inahitaji wachezaji waliofika angalau Robo Fainal ya Michuano ya CAF ili msimu ujao waweze kutuvusha tulipoishia msimu huu”
“Dhamira yetu ni kuwa na kikosi bora, baada ya kujifunza mambo mengi msimu huu ambao umekua mbaya kwetu, tumepoteza mataji yote. Hivyo tunatarajia kuwa na mpango mzuri wa kukisuka vyema kikosi chetu, ili kurejesha tulichokipoteza msimu huu.”
“Kuna baadhi ya wachezaji tutawaacha na wengine wataendelea kuwa sehemu ya timu yetu, watakaosajiliwa wataungana na watakaowakuta ili kuunda timu ambayo tunaamini itakua imara kwa michuano ya ndani na nje ya Tanzania.” amesema Ahmed Ally
Mbali na Usajili wa Wachezaji, Simba SC inatarajia kuwa na Kocha Mkuu mpya kuanzia msimu ujao, baada ya kuachana na Kocha Franco Pablo Martin.
No comments
Post a Comment