Chande:Hakuna kodi ya chakula na mbogamboga zinazokwenda zanzibar
Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeeleza kuwa bidhaa za chakula
na mbogamboga halisi zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar hazitozwi kodi,
tozo na ushuru wa aina yoyote kwa mujibu wa sheria.
Maelezo hayo
yametolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), bungeni
jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chaani, Mhe. Usonge Hamad Juma,
aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kupunguza kodi, tozo na ushuru wa bidhaa
za chakula na mbogamboga kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ili kudhibiti
mfumuko wa bei wa bidhaa hizo.
Mhe. Chande
alisema kuwa bidhaa hizo hazitozwi tozo ya uchakataji nyaraka kwa
sababu hazihitaji kufanyiwa mchakato wa nyaraka katika mfumo wa forodha.
Alisema bidhaa za chakula zinazotozwa tozo ni zile zinazotoka viwandani ambazo hutozwa tozo ya uchakataji nyaraka za forodha
ya asilimia 0.6 tu kwenye thamani ya mzigo huo.
“Lengo la tozo hii ni kugharamia huduma ya
uchakataji wa nyaraka za forodha na hutozwa kwa wateja wote wanaotumia Mfumo wa
Forodha (TANCIS)”, alibainisha Mhe. Chande.
Wakati huohuo,
Mhe. Chande alisema Serikali kupitia Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za
kiukaguzi wa miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya
makampuni ya kimataifa kwa lengo la kuzuia upotevu wa mapato.
Alisema hayo
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina alijetaka kujua
namna ambavyo Serikali
imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma kati ya makampuni ya kimataifa.
Alisema hatua hizo
ni pamoja na kuendelea kuboresha
mifumo ya ndani ya ukusanyaji kodi kama vile Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za
Utoaji wa Risiti za Kielektroniki na Mfumo wa Kuwasilisha Ritani Kielektroniki.
“Kutoa mafunzo ya vitendo kwa watumishi katika
nchi mbalimbali zenye uzoefu wa kushughulikia miamala ya uhamishaji wa bei ya
mauzo ya bidhaa na huduma baina ya makampuni za kimataifa”aliongeza
Mhe. Chande.
Alisema kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa
kubadilishana taarifa kati ya Serikali ya Tanzania na nchi zingine pamoja na kuendelea kufanya
majadiliano na wadau mbalimbali ili kuona uwezekano wa kujiunga na Global
Forum on Tax Transparency na ubadilishanaji wa taarifa kwa lengo la kupanua
wigo wa upatikanaji wa taarifa pia
ni miongoni mwa hatua hizo.
No comments
Post a Comment