RITA yasajili na kutoa vyeti kwa watoto zaidi ya laki mbili Manyara
Mkuu wa mkoa wa
Manyara Makongoro Nyerere amewataka wananchi kujitokeza kuwaandikisha watoto
wao wenye umri chini ya miaka mitano kupata vyeti vya kuzaliwa.
Makongoro ametoa kauli hiyo
katika kikao cha Tathmini kuhusu utekelezaji wa mpango wa usajili wa vizazi kwa
watoto wa umri chini ya Miaka Mitano mkoani Manyara, kilichofanyika katika
ukumbi wa mikutano mkoani hapo.
Amesema Idadi ya watoto
waliosajiliwa katika mkoa wa Manyara imeongezeka kutoka asilimia 6.3 na kufikia
asilimia 80.2.
Mpaka sasa mpango wa usajili wa
watoto unatekelezwa katika mikoa 23 ya Tanzania bara na zaidi ya watoto milioni
7.5 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa ambapo idadi hiyo imewezesha
kuongeza kiwango cha usajili wa watoto kutoka 13% mwaka 2012 na kufikia 65%
mwaka 2021.
Naye Katibu Mkuu wizara ya katiba
na Sheria Mary Makondo amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali
kwa lengo la kuleta maboresho ya mfumo wa usajili kupitia Mkakati wa Kitaifa wa
Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu ambazo ni Vizazi, Vifo,
Ndoa, Talaka na Watoto wa Kuasili.
Aidha ameziagiza Halmashauri zote
za mkoa wa Manyara ambazo ndio zinataratibu usajili katika maeneo yao,kuanza
kutenga fedha katika bajeti zao ili kuendeleza utekelezaji wa mpango huo kwa
kuwa jukumu la usajili kwa sasa lipo juu yao kwa mujibu wa sheria.
Ameeleza kuwa Mpango wa Usajili
wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ni uthibitisho wa sehemu ya juhudi za
Serikali kuhakikisha watoto wanasajiliwa na kupata nyaraka ya awali na ya
msingi ya utambulisho ambayo ni cheti cha kuzaliwa.
Aidha ameahidi,wizara yake
itaendelea kutoa ushirikiano kila itakapohitajika ili kuhakikisha mafanikio
yaliyopatikana yanadumishwa kwa kuendeleza upatikanaji wa huduma.
Makondo, Kwa niaba ya serikali amewashukuru
wadau wa maendeleo ambao ni shirika la umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto
duniani (UNICEF),Serikali ya Canada na kampuni ya simu za mkononi ya TIGO kwa
kuendelea kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.
Akizungumza katika kikao hicho
cha Tathmini, Kabidhi Wasii mkuu na afisa mtendaji mkuu wa wakala wa
Usajili,Ufilisi na udhamini (RITA) Angela Anatory, amesema mpango huo ulianza
mwezi mei 2021.
Kwa mujibu wa takwimu,tangu
mpango wa usajili ulipoanza kutekelezwa katika mkoa wa Manyara,zaidi ya watoto
259,317 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa sawa na asilimi 80.2 ya lengo
ambapo kabla ya kuanza mpango huo ni asilimia 6.3 tu ya watoto walikuwa
wamesajiliwa na kupata vyeti, hivyo kuna ongezeko la asilimia 73.9.
Amesema utekelezaji wa mpango huo
umeleta maboresho makubwa katika mfumo wa usajili wa vizazi na kutoa vyeti vya
kuzaliwa kwa watoto kwani kwa sasa huduma zinapatikana katika ofisi zote za
watendaji kata na vituo vya tiba.
No comments
Post a Comment