Wakati bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23 ikitarajiwa kusomwa wiki ijayo (Juni 14, 2022), baadhi ya wadau wamesema wanatarajia kuona ruzuku katika mafuta ikiendelea ili mwananchi apate ahueni.

Wamesema, wanatarajia kuona Serikali ikiainisha mbinu zaidi zitakazotumika kukuza matumizi ya gesi asilia kama nishati mbadala ya mafuta katika magari na viwanda vingi nchini.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Mwananchi juu ya matarajio yao kuelekea wa bajeti ya Serikali, hususan katika upande wa nishati.

 Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema wanatarajia kuona Serikali ikiendelea kutoa ruzuku katika mafuta ili kupunguza makali ya bei kwa watumiaji wa mwisho.

Alisema bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia bado haijashuka hivyo anatarajia Serikali itaendelea kutoa ruzuku.

“Mafuta ni bidhaa ya kimkakati na muhimu, Serikali ikiendelea na jitihada kama iliyozifanya mwezi huu kuhakikisha mafuta yanakuwepo kwa bei nafuu kwa mtumiaji wa mwisho itasaidia kuimarisha uchumi na kupunguza hatari ya kuwepo kwa mfumuko wa bei,” alisema Mgaya.

Dk Olomi Donath ambaye ni Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, alisema pia suala la bei ya mafuta linapaswa kutazamwa upya kwa kile alichokieleza kuwa kuendelea kuwa juu kunaweza kuchangia kupunguza ukuaji wa uchumi.

“Hili ni jambo ambalo linahitaji kuangaliwa, sijui kama bei itapunguzwa au la ila mafuta yakiendelea kuwa bei juu yanaweza kupunguza ukuaji wa uchumi,” Dk Olomi.

Mei mwaka huu, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema Serikali imetoa ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini, kutolewa kwa ruzuku hiyo hakutagusa miradi ya maendeleo inayoendelea.

“Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali. Ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini.

“Ruzuku hii ya Sh100 bilioni itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kuanzia Juni 1, 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa,” alisema Makamba.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa uchumi na biashara na mafuta, Dk Donath Olomi Tanzania hivi sasa inapaswa kuwekea mkazo matumizi ya gesi asilia.

Pia alisema ni vyema kuweka mkazo na kasi ya ujengaji wa vituo kwa ajili ya gesi asilia katika magari na kuongeza usambazaji wake katika viwanda ili kupunguza matumizi ya mafuta katika maeneo hayo.

“Vituo vya kujaza gesi asilia katika magari vijengwe vingi, hususan katika miji mikubwa kama ilivyokuwa kwa vituo vya mafuta, viwanda pia viunganishwe na nishati gesi asilia ili kupunguza makali,” alisema Dk Olomi.

Kuhusu umeme

Katika umeme, alitaka kuwekwa kwa sera zitakazowezesha uzalishaji wa umeme kwa kutumia njia mbadala kama maji ili kuifanya nchi kuwa na umeme wa kutosha na kutoka vyanzo tofauti.

Lakini pia alitaka utekelezaji wa bajeti ufanyike kikamilifu kwa kutoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji miradi kwa kile alichokieleza kuwa baadhi ya fedha zimekuwa zikitolewa wakati mwaka unakaribia kwisha na nyingine hazitoki kabisa.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abeli Kinyondo alisema wanatarajia kuona mikakati iliyotajwa na waziri inatekelezwa, huku akisema ujenzi wa miundombinu uliotajwa anaamini utatekelezwa ipasavyo.

Pia alisema moja ya vitu anavyotamani kukiona ni namna serikali ilivyojipanga kuanza kutoka katika matumizi ya mafuta na kuhamia katika matumizi ya nishati nyingine katika shughuli tofauti.

“Hili halijazungumzwa kwa ukubwa, halijafikiriwa,” alisema Dk Kinyondo.

Alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Makamba aliliomba Bunge kuidhinishia Sh2.905 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 ambapo kati yake Sh2.823 trilioni ikielekezwa katika miradi ya maendeleo.

Makamba alisema kati ya fedha hizo, Sh2.67 trilioni zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

“Katika mwaka 2022/23 Wizara ya Nishati imejipanga kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Nishati, lengo likiwa ni kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi asilia zilizopo nchini zinachangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa letu na watu wake na kuimarisha upatikanaji wa nishati,” alisema.

Alisema wizara yake itaendelea kutatua kero za wananchi, hususan upatikanaji wa nishati ya umeme pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma.

Tanesco yahitaji Sh4.42 tril

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imesema ili kuhakikisha nchi inaondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara inahitajika Sh4.42 trilioni ili kukamilisha uboreshaji wa gridi ya Taifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dustan Kitandula aliyasema hayo wakati akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2022/23.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) inaombewa Sh400 bilioni kwa ajili ya kuanza kazi ya kuboresha gridi ya Taifa. Kamati inasihi fedha hizi zitoke zote na kwa wakati,” alisema.

Alishauri kuwa utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu na Gridi kwa ujumla uendelee ili kuhakikisha miundombinu ya umeme inakuwa vizuri wakati wote.

Alisema Serikali ione namna ya kuiwezesha Tanesco kulilipa Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) Sh512.16 bilioni inazodaiwa.

“Serikali izisimamie wizara na taasisi za umma zinazodaiwa na Tanesco madeni ya ankara za umeme kwa muda mrefu yenye thamani ya Sh444.59 bilioni yaweze kulipwa ili Tanesco iweze kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.