TBS yatoa elimu ya viwango maadhimisho ya kitaifa wiki ya maziwa Katavi
Afisa Viwango (TBS),Bw.Joseph Tarimo akitoa elimu kwa wadau waliotembelea banda la TBS katika maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya maziwa yanayofanyika katika viwanja vya azimio mkoani Katavi.
Wazalishaji wa maziwa na bidhaa zake wameshauriwa kuthibitisha ubora wake hatua, ambayo itawasaidia kuwaongezea masoko na tija kwenye bidhaa hizo
Ushauri huo umetolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Azimio mkoani Katavi kuanzia Mei 27 na kumalizika Juni 1, mwaka huu.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Afisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, aliwataka washiriki hao kuhakikisha wanathibitisha ubora wa maziwa na bidhaa zake hatua ambayo itawasaidia kuwaongezea masoko na tija kwenye bidhaa zao.
Alisema TBS imeshiriki maonesho haya kwa lengo la kuwasogezea huduma karibu wazalishaji wa maziwa kwa kuwapatia elimu ya viwango ili waweze kuzalisha bidhaa bora na salama zinazoweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Hiyo ni kwa sababu nchi za Afrika Mashariki zina makubaliano kuhusiana na bidhaa zilizothibitishwa ubora ambapo kila mzalishaji aliyethibitisha ubora wa bidhaa yake ni ruksa kupeleka bidhaa hizo katika nchi yoyote katika ukanda huo bila kukumbana na vikwazo vya kibiashara.
“Huduma ya uthibitishaji ubora wa bidhaa kwa wajasiriamali wadogo ni bure kabisa, kinachotakiwa ni wajasiriamali kupata barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na kuipeleka TBS, ambapo mchakato wa kuwapatia alama ya ubora unaanza mara moja,” alisisitiza Mtemvu.
Alisema TBS inatambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi wengi, ndiyo maana kuna mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali kwa kuwa na hilo ni sehemu ya majukumu ya shirika ili waweze kupata alama ya ubora.
Aidha, alisema kupitia maonesho hayo walitoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala ya viwango na kuwataka waelewe kwamba vita ya bidhaa hafifu sio ya TBS pekee, bali ni jukumu la kila mwananchi.
Alisema wananchi hao walielimishwa umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku pamoja na kuwafahamisha fursa ya huduma ya kuthibitisha bure bidhaa za inayotolewa kwa wajasiriamali wadogo.
Kwa mujibu wa Mtemvu, mbali ya kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusu masuala ya viwango wametakiwa kuhakikisha wanakuwa mabalozi kwa kuhamasisha kutumia bidhaa bora katika jamii wanazoishi. Aliwataka wananchi waoliofika kuhudhuria maonesho hayo kutoa taarifa kwa shirika hilo pindi wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko.
No comments
Post a Comment