Header Ads

Header ADS

Waziri Mkuu awapa maagizo TAMISEMI

 


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemuagiza Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa na viongozi wengine wa wizara hiyo wahakikishe kuwa suala la ukusanyaji mapato kwenye Mikoa, Halmashauri na Mamlaka za Serikali za Mitaa linapewa kipaumbele ili kuongeza mapato ya Serikali.

Ametoa wito huo leo alipokutana na Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za wizara hiyo kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kuwakumbusha wajibu wao.

“Ni lazima ujitambue wewe ni nani hapa kwenye wizara, unatakiwa kufanya nini, mpango kazi wako ukoje na je ni wako peke yako ama unahitaji watu wengine ili uweze kuutekeleza,” amesema.

Ameongeza “Ajenda ya ukusanyaji mapato iwe ya kudumu ili yaongezeke hadi kufikia shilingi trilioni 2 kutoka makadirio ya sasa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Halmashauri zimekadiria kukusanya mapato ya ndani ya shilingi trilioni 1.01 ikilinganishwa na shilingi bilioni 863.85 zilizoidhinishwa kwa mwaka 2021/2022.
 
Amesema watumishi hao wanapaswa kutambua kwamba bila uaminifu, uadilifu na uwajibikaji hawawezi kufanikiwa lakini pia wanapaswa kusimamia mambo hayo matatu.

“Taarifa ya CAG kuhusu Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imebainisha Halmashauri 178 sawa na asilimia 96 zimepata hati safi, Halmashauri sita sawa na asilimia tatu zimepata hati zenye shaka na Halmashauri moja sawa na asilimia moja imepata hati mbaya,” ameongeza Waziri Mkuu.

Aidha ameitaka menejimenti ya wizara hiyo iwe na ubunifu, iongeze matumizi ya TEHAMA ili kuongeza mapato ya Serikali, Wakuu wa Idara wagawe majukumu kwa wasadizi wao na wakurugenzi wawe na vikao vya mara kwa mara na wasaidizi wao.

No comments

Powered by Blogger.