Makinda : kwenye sensa tutakusanya taarifa za kaya siyo familia,wapangaji ni kaya
Kamisaa
wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda ambaye ni Spika
Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekutana na kuzungumza na
wadau mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Julai 4,2022 katika ukumbi wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Shinyanga
yenye lengo la kutoa elimu ya Sensa na kuhamasisha wananchi kushiriki
kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23,2022.
Akizungumza
na wadau hao Makinda amesema maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yanaendelea
vizuri huku akisisitiza Uzalendo kwa wananchi ili kufanikisha zoezi hili ikiwa
ni pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa Makarani wa Sensa.
Makinda
ameagiza elimu na hamasa ya Sensa ya watu na makazi iendelee kutolewa kila
mahali hadi siku ya Sensa Agosti 23,2022 ili kuhakikisha kila mwananchi anapata
taarifa na kuelewa kuhusu Sensa kwa maendeleo ya taifa.
"Siku ya sensa wananchi wanatakiwa kutoa taarifa za ukweli. Msiwafiche watu wenye ulemavu",amesema Makinda.
"Sensa ya watu na makazi itafanyika Tarehe 23 Agosti. Mkuu wa kaya awe na taarifa za watu waliolala usiku wa Agosti 23,2022. Taarifa za watu wenye ulemavu zikusanywe ili kusaidia serikali kupanga mipango kwa watau wenye ulemavu ili wapate huduma wanazotakiwa wapate",ameongeza.
"Makarani wa Sensa watafika katika kila kaya.
Kwa wale wapangaji wako katika nyumba hizo ni kaya, wewe mwenye nyumba siyo
kaya. Mpangaji kwenye nyumba yako atahesabiwa kuwa ni kaya. Kila mtu
aliyelala ndani ya mipaka ya Tanzania atahesabiwa",amesema Makinda.
Naye
Mtakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Pastory Ulimali amesema Dodoso
la Sensa litakusanya taarifa za kaya siyo familia huku akibainisha kuwa
siyo lazima mkuu wa kaya awe baba au mama, mkuu wa kaya anaweza kutoa maelekezo
kwa mtu mwingine katika kaya kwa niaba ya mkuu wa kaya ili kutoa taarifa kwa
makarani wa sensa watakaotembelea kaya husika.
"Sensa hii inawahusu watu wote awe mgeni au
mwenyeji, ilimradi huyo mtu amelala ndani ya mipaka ya Tanzania usiku wa Agosti
23,2022, Kila mtu atahesabiwa. Kila mtu ahesabiwe mara moja tu na kila mmoja
afanye uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ili zoezi hili lifanyike
kikamilifu. Na kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mbali ya kuhesabu watu pia
tutahesabu majengo tukitumia vifaa vya kidigitali - Vishikwambi",amesema
Ulimali.
No comments
Post a Comment