TARURA Namtumbo yaishukuru serikali kutoa fedha za ujenzi wahaidi kujenga miradi yenye viwango
Wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura)
wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,umeishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa
kuipatia jumla ya Sh.milioni 495,000,000 kwa mwaka wa fedha 2020/2021
zilizotumika kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Meneja wa Tarura wilaya ya Namtumbo
Mhandisi Fabian Lugalaba, wakati akizungumza kuhusiana na barabara mpya
zilizojengwa na Tarura ambazo zimewezesha kuunganisha vijiji mbalimbali
na kuchochea uchumi wa wananchi.
Lugalaba alisema, kati ya fedha hizo Sh.milioni 90,000,000 zimetumika kwa
ajili ya kujenga(kutoboa) barabara mpya na kiasi cha Sh.milioni
405,000,000 zimetumika kujenga madaraja yaliyowezesha kurudisha
mawasiliano kwa vijiji vya Mgombasi,Miembeni na Likuyumandela.
Kwa mujibu wake,katikati ya kata ya Mgombasi na Likuyuseka kuna kijiji
cha Miembeni ambacho hakikuwa na mawasiliano ya barabara,hivyo kusababisha
wakazi wake kuwa na mazingira magumu pindi wanapohitaji kwenda maeneo mengine
kwa ajili ya kupata huduma ikiwamo ya afya.
Alisema,kutokana na changamoto hiyo serikali iliona umuhimu wa
kupeleka barabara katika maeneo hayo ambapo katika bajeti ya mwaka wa
fedha 2020/2021 ilitenga jumla ya Sh.milioni 90 kwa ajili ya
kutoboa(kujenga)barabara mpya itakayounganisha kata hizo na kijiji hicho.
Lugalala alitaja barabara hizo ni Mfuate-Miembeni-Mgombasi yenye
urefu wa km 17.2 iliyogharimu juma ya Sh.milioni 50 na barabara ya
Likuyumandela-Miembeni yenye urefu km 11.5 iliyojengwa kwa gharama
ya Sh.milioni 40.
Aidha alisema,katika maeneo hayo yote mawili kuna mito ambayo
ilihitaji kujengwa madaraja,ambapo katika barabara ya Mfuate-Miembeni- Mgombasi
kulihitaji daraja la mita 20 katika mto Luegu na limejengwa kwa gharama ya
Sh.milioni 350.
Lugalaba alitaja daraja lingine ni la mita 8 linalounganisha
kijiji cha Miembeni kwenda Likuyumandela ambalo hadi kukamilika
limegharimu sh.milioni 40.
Alieleza kuwa,kwa kutumia fedha zinazoletwa na Serikali zikiwamo za
ongezeko la tozo zilizoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, watahakikisha
wanajenga miradi ya barabara kwa ubora wa hali ya juu,uaminifu,uadilifu na
inayoendana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa ili wananchi wengi hasa
waishio maeneo ya vijijini wafikiwe na mtandao wa barabara.
Alisema,malengo ya Tarura ni kuhakikisha maeneo yote ambayo hayafikiki
kwa urahisi wanatumia fedha zinazotengwa na Serikali kufikisha huduma ya
mawasiliano ya barabara ili kuwarahisishia wananchi kufanya shughuli zao za
maendeleo.
Amewaomba wananchi ambao barabara na madaraja yamejengwa,kuhakikisha
wanatunza miundombinu hiyo na kila mmoja kuwa mlinzi kwa mwenzake ili iweze
kudumu na kwa muda mrefu.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Likuyumandela,Mfuate na Miembeni,
wameishukuru serikali kwa jitihada za kurudisha mawasiliano ya barabara
katika maeneo hayo.
Ali Mtima mkazi wa kijiji cha Miembeni alisema,kabla ya kujengwa kwa
daraja katika mto Luegu linalounganisha kijiji hicho na Mgombasi,walilazimika
kupita kwa shida katika mto huo wenye maji mengi hasa kipindi cha masika.
Mtima alisema,baadhi ya watu wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji pindi
wanapohitaji kwenda kijiji jirani cha Mgombasi kufuata huduma mbalimbali za
kijamii ikiwamo huduma za afya.
Issa Amir mkazi wa Mgombasi, ameishukuru Tarura kwa kujenga barabara
zinazounganisha kata ya Mgombasi na Likuyu kwani zimerahisisha mawasiliano na
kuchochea kukua kwa uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
Alisema baada ya kujengwa kwa barabara hizo, sasa wanasafirisha mazao kutoka mashambani kwenda sokoni kwa urahisi na wafanyabiashara wengi wanafika kwa ajili ya kununua mazao wanayozalisha.
Daraja la mto Lumbegea linalounganisha kijiji cha Miembenina kijiji cha Likuyumandela lililojengwa na Tarura wilaya ya Namtumbo likiwa limekamilika na kuanza kutumika.
Mhandisi wa wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilayani Namtumbo Samwel Makongwa kushoto na mfanyakazi wa Tarura Hassan Nyoni wakiwaongoza baadhi ya wananchi wa kijiji cha Likuyumandela kuangalia daraja la Mto Lumbegea.
Muonekano wa daraja la mto Luegu lililojengwa na Tarura wilaya ya Namtumbo linatajwa kuwa na mchango mkubwa kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kutokana na vijiji vinavyounganishwa na daraja hilo kuwa na uzalishaji mkubw wa mazao ya chakula na Biashara.
Mhandisi wa Tarura wilayani Namtumbo Samwel Makongwa kushoto na mfanyakazi wa Tarura Hassan Nyoni wakikagua kingo za daraja la Mtu Luegu linalounganisha kijiji cha Miembeni na Mgombasi wilayani humo ambalo linatajwa kukamilika kwake litaharakisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
barabara inayounganisha kijiji cha Miembeni-Mgombasi kama inavyoonekana baada ya kujengwa na wakala wa barabara za mijijini na vijijini(Tarura)wilayani Namtumbo
No comments
Post a Comment