JAFO atoa maagizo kigoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameagiza shughuli za ujenzi wa miundombinu ya makazi zizingatie masuala ya kimazingira.
Ametoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kikazi mkoani Kigoma kukagua shughuli za mazingira katika eneo la Mlima Mlole, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Dk.Jafo alisema kuwa vibali vya ujenzi viainishe takwa la kuweka mfumo wa uvunaji wa maji ya mvua sambamba na upandaji miti katika makazi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo wakati mvua zinapo nyesha.
“Kikubwa maafisa wa manispaa wahakikishe wanawaelekeza wananchi hawa waliopewa maeneo haya kuhusu utaratibu wa kuyaendeleza na kujenga miundombinu yenye kukidhi matakwa ya kimazingira,” alisema.
Aidha, Waziri Jafo amesema Serikali kwa kutumia wataalamu wa Bandari pamoja na Mazingira wamejiridhisha kutowepo kwa athari za kimazingira katika Bandari ya Kigoma hivyo ameidhinisha uendelezaji wa makazi katika eneo hilo.
Hatua
hiyo inakuja baada ya kuimarishwa kwa kuta za Mto Rubengela uliokuwa ukisababisha mmomonyoko wa ardhi nyakati za mvua na kuingiza tope na mchanga eneo la bandari.
Pia, waziri huyo aliwataka wataalamu wa mazingira kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wafuate sheria na kuepuka na changamoto zinazoweza kutokea katika maeneo yao.
Itakumbukwa zuio la kuendeleza makazi lilitolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari mkoani Kigoma mwaka 2009 kuwataka wakazi wa eneo hilo kusitisha ujenzi wa nyumba pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.
Katazo hilo lilitolewa ili kusubiri kufanyika kwa utafiti ambapo Serikali ilikuja na suluhisho la kuanza kujenga kingo za mto huo hatua iliyosaidia kupunguza mmomonyoko wa ardhi katika eneo hilo.
No comments
Post a Comment