Header Ads

Header ADS

Serikali yaeleza sababu ya Wananchi kujichukulia sheria mkononi

Serikali imesema sababu za wananchi kujichukulia hatua mkononi na kuongeza mauaji nchini ni wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, ulevi na imani za kishirikini.

Akijibu swali Bungeni kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Septemba 14, 2022, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Hassan Chande, amesema katika kudhibiti wimbi hili waliunda timu maalum ya kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Chande amesema pamoja na kuchukua hatua za kisheria kama zilivyopendekezwa na timu waliyoiunda, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi.


Amesema elimu hiyo imekuwa ikitolewa  kwa kuwashirikisha viongozi wa siasa, dini, wazee wa mila na watu wanaoheshimika kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, katika kutatua migogoro na migongano katika jamii.

Baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema licha ya Serikali kuchukua hatua bado tatizo hilo linaendelea kukuwa hivyo kuitaka serikali kuangalia hatua za kawaida.

“Na mtuulize sisi watu wa kawaida kabisa tunafikiri hilo jambo linaweza kumalizwa kwa namna gani kwasababu kadri linavyozungumzwa utasikia leo huku, kesho huku, sasa huenda linatembea kwasababu linazungumzwa na watu wazito,” amesema Spika Tulia.

Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge George Simbachawene amesema iko haja ya kushirikiana na wadau wote katika kukabiliana na changamoto hiyo.

“Law enforcers (wasimamizi wa sheria), tujiulize tunatimiza wajibu wetu sawa sawa, kama kunatokea hasira ya wananchi kuchukua hatua mkononi kwanini wanachukua hatua mkononi? Ni wapi hapako sawa,”amesema.

Awali Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso alitaka kufahamu nini kauli ya Serikali katika kutatua changamoto ya wimbi kubwa la mauaji hapa nchini Tanzania.


No comments

Powered by Blogger.