Urusi kuitisha kikao ha baraza la usalama
Urusi inapanga kuitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uharibifu uliofanywa katika mabomba mawili ya gesi ya chini ya bahari ya Nord Stream 1 na 2.
Hayo yamesemwa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye mtandao wa Telegram.
Utawala wa Kremlin umekanusha tuhuma kwamba una dhima kwenye uvujaji wa gesi katika mabomba hayo. Msemaji wa rais wa Urusi Vladimir Putin, Dmitry Peskov amesema ni "jambo la kutabirika, ni ujinga na upuuzi kuwa na mawazo kama hayo".
Peskov amesema ni muhimu kusubiri uchunguzi katika maeneo yanayovuja na kubaini kama uharibifu huo ulisababishwa na mlipuko ama la. Peskov pia amesema si kwa maslahi ya Urusi kwa gesi inayopitia kwenye mabomba hayo kuhujumiwa, akisema gesi inasukumwa kwenye njia zote za bomba la Nord Stream 2.
No comments
Post a Comment