Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Lami Mikoa ya Tabora na Kigoma wafikia asilimia 66
Mradi wa ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha Mikoa ya Tabora na Kigoma kipande cha Kazilambwa-Chagu chenye urefu wa km 36 umefikia asilimia 66 na utekelezaji wake unaendelea kwa kasi kubwa.
Akizungumza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Raphael Mlimaji alisema mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya STECOL kutoka China kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Kimataifa (OPEC) na Serikali ya Tanzania.
Alisema utekelezaji mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwakani na hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh bil 32.
Alibainisha km 26 za mradi huo zipo upande wa Tabora eneo la Kaliua na km 10 upande wa Kigoma, hivyo akatoa wito kwa jamii inayoishi kando kando ya eneo la mradi kutunza miundombinu itakayowekwa ikiwemo alama za barabarani na taa.
Mhandisi Mlimaji alisisitiza kuwa mradi huo ni muhimu sana kwa kuwa utamaliza kero ya muda mrefu kwa wakazi wa Mikoa hiyo kwa kuwa utarahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa na mazao yao.
Aliongeza kuwa mazungumzo na Mfadhili yanaendelea ili kuangalia uwezekano wa kuongeza km 11.4 za barabara ya mchepuko kipande cha Ugansa-Usinge (km 7.4) na kipande cha barabara ya zamani ya Chagu-Ugansa (km 4).
Alibainisha kuwa kama wataafikiana vizuri kiasi cha sh bil 14 ambazo ni salio la gharama nzima ya mradi zitatumika kujenga vipande hivyo 2 kwa kiwango cha lami ili kuwezesha wakazi wa maeneo hanufaika na mradi huo.
Aidha aliongeza kuwa serikali inaendelea na mchakato wa ujenzi wa km 172 za barabara ya lami kutoka Ipole (Tabora) hadi Rungwa ambayo ni kiunganishi muhimu kwa Mikoa ya Tabora na Mbeya.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora Mhandisi Raphael Mlimaji ( wa kwanza kulia) akiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia) kwenye ziara maalumu ya kukagua ujenzi za barabara ya Kazilambwa-Chagu yenye urefu wa km 36 inayounganisha Mkoa wa Tabora na Kigoma hivi karibuni .
No comments
Post a Comment