Timu ya Wanawake ya Tanzania Serengeti Girls itacheza 22 Oktoba 2022 dhidi ya Colombia
Timu ya Taifa Tanzania ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls itacheza Robo Fainali Kombe la Dunia dhidi ya Colombia, Oktoba 22 katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru.
Serengeti Girls imetinga hatua hiyo, kufuatia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Canada ilioyapata jana Jumanne (Oktoba 18) nchini India zinapoendelea Fainali hizo.
Sare hiyo imeifanya Serengeti Girls kufikisha alama nne zinazoiweka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D, huku Japan ikiongoza msimamo wa Kundi hilo kwa kufukisha alama tisa.
Canada na Ufaransa zimeondoshwa kwenye Fainali hizo kupitia Kundi D, zikimaliza nafasi ya tatu na nne.
Serengeti Girls iliweka matumaini ya kufuzu Robo Fainali, baada ya ushindi dhidi ya Ufaransa siku ya Jumamosi (Oktoba 15), hivyo matokeo ya sare dhidi ya Canada na Japan kushinda dhidi ya Ufaransa yaliivusha timu hiyo ya Tanzania.
Colombia inakutana na Serengeti Girls, baada ya kuongoza Kundi C ikiwa na alama sita sawa na Mabingwa watetezi Hispania iliyozidiwa uwiyano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Michezo mingine ya Robo Fainali Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 17, itashuhudia Marekani ikicheza dhidi ya Nigeria Oktoba 21 katika Uwanja wa DY Patil mjini Mumbai, huku siku hiyo hiyo Ujerumani itaikabili Brazil.
Kikosi cha Japan kitacheza dhidi ya Mabingwa watetezi Hispania Oktoba 22 katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru mjini Margao, ambao pia utashuhudia Tanzania ikipapatuana na Colombia siku hiyo.
No comments
Post a Comment