Walimu watakiwa kufanya kazi zao kwa ufanisi bila kuingiliwa na Wanasiasa
WalimuWilayani Simanjiro Mkoani Manyara wametakiwa kufanya kazi zao kwa ufanisi na bila hofu kwani hakuna mwanasiasa atakayeingilia taaluma yao.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer ameyasema hayo wakati akipokea salamu za pongezi kwa kushinda nafasi hiyo na kupatiwa keki ya ushindi na viongozi wa chama cha walimu nchini (CWT) wilayani Simanjiro.
Kiria amesema katika kipindi chake akiwa Mwenyekiti wa CCM walimu wa Simanjiro hawatanyanyaswa na mwanasiasa yeyote au mtumishi yeyote wa serikali.
“Serikali iliyopo madarakani ni serikali inyoongozwa na CCM hivyo fanyeni kazi yenu ya taaluma bila kumuhofia mtu yeyote au jambo lolote lile kwani walimu tunawategemea mno,” amesema Kiria.
Mwenyekiti wa CWT wilayani Simanjiro mwalimu Abraham Kisimbi amempongeza Kiria kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM wa wilaya ya Simanjiro.
Mwalimu Kisimbi amesema wameamua kumpongeza Mwenyekiti huyo mpya wa CCM na kujitambulisha kwake kwani wao wamepangisha ofisi zake kwenye jengo la CCM.
“Pia tunakukaribisha kwenye mkutano wetu wa CWT wilaya ya Simanjiro ambapo pia kutakuwa na harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya chama chetu,” amesema mwalimu Kisimbi.
Katibu wa CWT wilaya ya Simanjiro mwalimu Nazama Tarimo amesema walimu wana matarajio makubwa kwa Kiria kwani ni kiongozi mwenye maono.
No comments
Post a Comment