Header Ads

Header ADS

Hamad Masauni ameliagiza jeshi la polisi kuwakamata wafugaji waliohusika na mauaji ya watu 12

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kipindimbi, Kata ya Njinjo, Wilayani Kilwa Mkoani Lindi, leo Novemba 1, 2022, ambapo amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata walioua watu 12 kutokana na mgogoro wa wakulima na wafugaji Mkoani Lindi. Kushoto ni Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini, CP Awadhi Haji, na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kipindimbi, Kata ya Njinjo, Wilayani Kilwa Mkoani Lindi, leo Novemba 1, 2022, aambapo amewataka wafugaji mkoani humo kuacha kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima. Mgogoro wa wakulima na wafugaji umesababisha vifo vya watu 12 mkoani humo. 

Diwani wa Kata ya Kikole, Mussa Kinjokwile akiwasilisha kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni (hayupo pichani) malalamiko ya wananchi kuhusu wafugaji waliovamia katika Kata hiyo na kusababisha kifo cha mkulima mmoja katika Kata hiyo, Wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi, leo Novemba 1, 2022. Mgogoro wa wakulima na wafugaji Mkoani humo umesabisha vifo vya watu 12. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kilwa, Mkoani Lindi wakati alipowasili Wilayani humo kwa ajili ziara ya kikazi, leo Novemba 1, 2022.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kushoto), akimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) alipokuwa akimfafanulia jambo wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kikole, Wilayani Kilwa Mkoani Lindi, kuhusu mgogoro wa wakulima na wafugaji uliosababisha vifo vya watu 12 Mkoani humo. Kushoto ni Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini, CP Awadhi Haji, na wapili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata mara moja wafugaji waliohusika katika mauaji ya watu 12 Mkoani Lindi.

Masauni ametoa kauli hiyo akiwa ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi katika Vijiji vya Kikole, Kipindimbi na Zinga Kibaoni Wilayani Kilwa, Mkoani humo Oktoba 31, 2022, katika ziara yao kufuatia mgogoro wa wakulima na Wafugaji mkoani humo.

Alisema Serikali haiwezi kukaa kimya wakati matukio hayo ya kinyama yakiendelea na haitakubali kuona mfugaji au mkulima anavunja sheria, amani, hivyo lazima sheria ifuatwe na atakayekiukwa atashughulikiwa.

“Natoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watu wote nchi nzima walioshiriki kuua watu wengine, ikiwemo hawa walioua wakulima katika Wilaya hii ya Kilwa na Wilaya zingine za Mkoa huu wa Lindi ambazo tunakwenda kwanza wakamtwe, ninashangaa mpaka leo hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa, inatutia mashaka makubwa,” alisema Masauni na kuongeza;

“Kamishna upo hapa na RPC upo hapa hakikisheni hawa mnawakamata haraka ili iwe fundisho kwa watu wengine, haiwezekani mtu anaua raia kama anaua kuku, watu 12 wamekufa katika mkoa huu wa Lindi, hawa ni binadamu, leo ameua mmoja akamatwi, kesho kaua mwingime hakamtwi, naa hata waliofanya uhalifu kuiba au kujeruhi nao wakamatwe.”

Aliongeza kuwa kwa yeyote ambaye ameshiriki katika kusababisha matatizo hayo ya vifo katika kutenda makusudi au kuzembea, kwa wale ambao wanaihusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na wengine ametaka kila mtu awajibike kwa nafasi yake na kila ambaye yupo chini ya Serikali kwa ujumla wake anataka wawajibike ipasavyo.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji waliopo katika vijiji ambavyo hawaruhusiwi kuwepo, waondoke katika maeneo hayo, waende katika vijiji vilivyopangwa kwa ajili ya mifugo.

“Nawataka wafugaji kuacha tabia ya kupeleka mifugo katika mashamba ya wakulima, marufuku kupeleka mifugo yenu katika maeneo ambayo hamruhusiwi ikiwemo katika Kijiji hiki cha Kikole, lazima utaratibu ufuatwe,” alisema Ndaki.

Naye Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini, CP Awadhi Haji amesema Jeshi la Polisi litafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwasaka wahalifu ambao wameua watu 12 katika Mkoa huo na watakamatwa na pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika msako huo.

“RPC {Kamanda wa Polisi Mkoa) ninaagiza kuanzia sasa lete askari kuja kuendesha msako nyumba kwa nyumba, ili tunataka hawa wananchi watembee kifua mbele kwenda shambani au wapi hata kwenda porini kule, mfugaji amekamatwa ahojiwe amekujaje kama Mwenyekiti amemuagiza kamata Mwenyekiti weka ndani chukua hatua kali, tusipofanya hivyo tutakuja kujuta nchi haitawaliki kwasababu ya tamaa ya watu wachache wasiotaka kuwa waadilifu katika maeneo yao ya kazi,” alisema CP Awadhi.

Mkazi wa Kijiji cha Kikole, Pili Mneka amesema kutokana na kifo cha mkulima mwenzao katika Kijiji hicho cha Kikole, Kata ya Kikole, Wilayani Kilwa, kimewaudhunisha na wanakosa amani kwa kuwa na uoga kutokana na wafugaji hao kufanya ukatili kwa mkulima mwenzao.

Waziri Masauni, Waziri Ndaki na viongozi wengine wanaendelea na ziara mkoani humo ambapo pia wanatarajia kutembelea Wilaya za Liwale na Nachingwea katika Mkoa huo kufuatilia matukio hayo ya mauaji ambayo yanasababishwa kwa sehemu kubwa na wafugaji.

No comments

Powered by Blogger.