Taratibu za mabadiliko ya sheria ya Habari bado hazijakamilika
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema, serikali ilishindwa kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari bungeni katika Bunge la Novemba mwaka huu, kutokana na baadhi ya taratibu kutokamilika.
Akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma Nape amesema Serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutani kutoka kwa wadau wa habari.
Amesema, haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.
Kuhusu takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape alisema, wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.
‘‘Katika Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Rais aliagiza wizara kutaka kukutana na wanahabari. Tunafanyia kazi hilo,’’ alisema Nape.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), James Marenga, alisema katika kikao cha pili, hakuna jambo litalobaki bila kushughulikiwa.
No comments
Post a Comment