Halmashauri ya Mji Njombe Kushirikiana na SIDO yatoa mafunzo ya kilimo Cha Uyoga
Halmashauri ya mji wa Njombe kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia viwanda vidogovidogo SIDO imetoa mafunzo ya kilimo kipya cha uyoga kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake,vijana na wazee huku lengo likiwa ni kuongeza idadi ya mazao ya biashara yatakayokuwa yakilimwa katika mji huo na kisha kutanua fursa za ajira kwa vijana
Mbali na kutanua wigo wa fursa katika kilimo ,halmashauri ya mji wa Njombe imelenga kuandaa vikundi vya ujasiriamali ambayo vitakuja kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake,Vijana na Walemavu .
Awali akizungumzia fursa kubwa iliyopo katika kilimo cha Uyoga sokoni Christina Daniel ambaye ni ofisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya mji wa Njombe anasema ni kutokana na kuongezeka kwa mahitaji sokoni na kuadimika kwa mboga za majani .
Katika hatua nyingine Ofisa maendeleo huyo amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa kutoa elimu kwa vikundi wa wajasiriamali ili viweze kuwa na sifa ya kupata mikopo ya halmashauri yenye lengo la kuwashika mkono na kuendeleza biashara zao.
“Tuna utaratibu wa kutoa elimu kwa vikundi vya wajasiriamali na kisha baadae kuvipa mikopo ambavyo vinakuwa vimekidhi sifa ya kupata mikopo,anasema Christina Daniel ofisa maendeleo halmashauri ya mji Njombe.
Nae Frank Bathurumeo ambaye ni kaimu meneja shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo Njombe SIDO kwa niaba ya maneje anasema shirika hilo limekuwa likifanya jitihada lukuki za kutafuta watalaamu na kisha kushirikiana na halmashauri kutoa elimu za ujasiriamali na mikopo yenye liba naafuu kwa wajasiriamali wadogo.
Bathurumeo amesema katika mwaka huu wa fedha SIDO Mkoa wa Njombe imetenga fedha kiasi cha zaidi ya mil 200 kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali na kisha kutoa rai kuchangamkia fursa hiyo.
Kwa upande wao wanufaika wa mafunzo hayo akiwemo Jakson Mwabena wamezungumzia kilichowasukuma kushiriki ambapo wanasema ni kutokana na kuongezeka kwa mahitaji sokoni huku pia wakisema kilimo hicho kinatumia eneo na maji kidogo huku pia wakisema faida kubwa zaidi iko pale ambapo mbolea za chumvichumvi hazitumii.
Katika hatua nyingine wanasema ujio wa kilimo hicho ni muarobaini wa tatizo la ajira kwa vijana.
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka mkoa wa Iringa Elias Mbuligwe amesema mbali na kilimo cha uyoga kuwa na fursa kwa wazalishaji kutengeneza uchumi wao lakini pia uyoga unafaida kubwa kimwili kwani una madini mengi ambayo yanapatikana katuka vyakula vingine yakiwemo ya Zinc na utajiri mkubwa wa Protini.
Katika mafunzo hayo ya siku tatu takribani wajasiriamali 30 wamefundishwa na kutunukiwa vyeti.
No comments
Post a Comment