Header Ads

Header ADS

Bashe ahakikisha kutatua changamoto za mfumo wa utoaji Ruzuku ya Mbolea

 

Waziri wa Kilimo  Hussein Bashe amesema Changamoto zilizopo kwenye mfumo wa utoji wa ruzuku ya mbolea ni za muda mfupi kwani mfumo huo umeanzishwa mwaka huu na mwanzo ni mgumu.

Amesema mfumo ni mzuri kwani unamtambua mkulima anayelengwa kunufaika na mbolea za ruzuku  tofauti na mfumo wa vocha uliotumika miaka ya nyuma na kunufaisha wafanyabiashara wa mbolea pekee.

“Mfumo wa mbolea ya ruzuku una changamoto zake lakini hatuwezi kurudi nyuma sasabu unamtambua mkulima” Waziri Bashe alikazia.

Waziri Bashe alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti  wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe akitembelea maghala ya mbolea na kukagua namna utoaji wa huduma ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima unavyoendelea pamoja na kuwasikiliza, kuzungumza na kutatua kero za wananchi.

Waziri Bashe amefafanua kuwa lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kumlipia ruzuku mkulima na kwa kutumia mfumo huo Serikali italipia mbolea iliyomfikia mkulima na si vinginevyo. 

Katika kutatua  changamoto ya misongamano Bashe amewaelekeza wauzaji wa mbolea kuongeza idadi ya watoa huduma za kuuza  ili kuweza kuwahudumia wakulima wengi kwa muda mfupi.

Waziri Bashe amewataka wakulima kuwa na subira na kubainisha kufikia  msimu ujao wa kilimo changamoto hizo hazitakuwepo.

“Mateso mnayoyapata ya foleni yatakwisha kuweni wavumilivu wakati serikali inajenga mfumo” Waziri Bashe alimaliza.

Aidha, waziri Bashe ameuomba uongozi wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe  kuwa waelimishaji wakubwa wa wananchi juu ya kutunza namba zao za utambulisho wa mkulima ili wasirubuniwe na kuziuza kwa mawakala wasiowaaminifu.

No comments

Powered by Blogger.